Header Ads

WABUNGE WATAKA BAJETI ZA MAENDELEO ZIELEKEZWE

 MuroTv

Wabunge wataka bajeti za maendeleo zitekelezwe

Ukumbi wa Bunge
UTOAJI wa fedha kidogo za bajeti katika fungu la maendeleo katika wizara mbalimbali nchini, umeibua mjadala mkubwa bungeni huku wabunge wengi wakisisitiza umuhimu wa bajeti za maendeleo kutekelezeka ili miradi isikwame.
Wameitaka serikali kuona umuhimu wa kutengeneza vipaumbele vichache na kuvipangia bajeti kulingana na fedha iliyopo ili kuepusha wabunge kupitisha bajeti ambayo haitekelezwi.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango ya mwaka wa fedha 2017/18 bungeni Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Josephat Kandege alisema hali ya utoaji fedha ya serikali kwa mafungu ya wizara yaliyopitishwa na Bunge hairidhishi.
Alitoa mfano kuwa Wizara ya Fedha ilitengewa Sh bilioni 791.9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi Machi mwaka huu ni Sh bilioni 18.89 zilitolewa kugharamia miradi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia mbili ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
“Wizara hii ikishindwa kuwajibika vyema, itasababisha kushindwa kufikia malengo kwa wizara nyingine,” alieleza. Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde, alisema utoaji finyu wa fedha za maendeleo umeonekana pia katika taarifa za kamati nyingi za Bunge. Aliishauri serikali kuweka malengo yanayotekelezeka.
Alisema katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira mwaka wa fedha wa 2016/17 ilipitishiwa na Bunge Sh bilioni 10.9 za miradi ya maendeleo, lakini zilitolewa Sh bilioni 1.2 sawa na asilimia 11 wakati Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliidhinishiwa Sh bilioni 35.3, lakini zilizotolewa ni Sh bilioni 2.9 (asilimia 8.4).
Alitaja Wizara ya Ujenzi kuwa ndiyo iliyovuka kiwango cha asilimia 50 kilichotolewa kwa fedha za maendeleo. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) alitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha za kutosha katika miradi ya maendeleo hususani katika wizara zilizopewa kipaumbele ili kufikia malengo.
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alipendekeza Bunge hilo liandae ratiba maalumu kwa ajili ya wabunge kwenda sehemu mbalimbali kutafuta vyanzo vya mapato ya nchi kwa jumla badala ya wabunge kubaki kujadili matumizi ya serikali.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), aliitaka serikali itengeneze mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuweka kodi zinazovumilika na vivutio vinavyoeendana na sekta nyingine ili kukuza uchumi wa nchi.

No comments:

Powered by Blogger.