Header Ads

MAGHEMBE AWAPONGEZA KAGERA KUONDOA MIFUGO HIFADHINI

MuroTv

Maghembe awapongeza Kagera kuondoa mifugo hifadhini

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kuondoa mifugo katika hifadhi na kuonya watumishi watakaoruhusu mifugo hiyo kurudi, watafukuzwa kazi.
Maghembe alitoa pongezi na tahadhari hiyo jana mjini Bukoba wakati akizungumza na uongozi wa mkoa huo unaoongozwa na Meja Jenerali mstaafu, Salim Kijuu. Alisema kazi hiyo ni ya kupongezwa kwa kuwa imeleta matumaini ya uhifadhi mkoani Kagera na taifa kwa ujumla.
“Ninawashukuru kwa jinsi mlivyofanya ile operesheni ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi zetu. Tulifanya kwa weledi, hata kama watu wanalalamika, hakuna aliyesema kuku wangu waliuawa, walipigwa risasi, tulinyang’anywa mifugo, kazi hii ilifanywa vizuri na kwa weledi mkubwa,” alisema.
“Hatutaruhusu tena mifugo hiyo irudi huko ndani ya hifadhi. Hili ni jambo kubwa ambalo ni wajibu wa wahifadhi wote kuhakikisha hakuna mifugo itakayokuwa inaingia humo ndani. Kuanzia sasa kama utakuta mtu ameingia kwenye hifadhi yako, tunamwondoa yeye na familia yake yote ili mbegu yake mbaya isibaki katika uhifadhi wa wanyamapori,” alisema.
Alisema ili kuimarisha ulinzi katika hifadhi hizo, utaratibu wa kutumia ndege maalumu za doria na ‘drones’ (ndege zisizo na rubani) utawekwa ili kuwabaini wahalifu wanaokaidi agizo hilo wachukuliwe hatua za kisheria.
“Tutakuwa tunarusha ndege mara moja kila baada ya wiki tatu au wiki mbili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaingia na mifugo humo ndani. Pili tutafanya doria na ndege zile ambazo hazina marobani kuhakikisha kwamba tunaangalia kinachotokea humo ndani wakati wote, “ alisema.
“Najua wanaweza kubadilisha system (utaratibu) ikawa ya usiku na hawa askari hawa tutawapa mafunzo maalumu chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kuanzia miezi sita mpaka tisa, wajifunze namna ya kuhangaika na hawa wanaoingia kwenye hifadhi zetu,” alisema Waziri.
Akizungumzia operesheni hiyo, alisema ulitolewa muda maalumu kwa watu kutoa mifugo yao kwa hiari katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu mkoani humo, na waliotii hakuna mashitaka yalifunguliwa dhidi yao.
Alisema wale waliokaidi walifikishwa mahakamani na mifugo yao ikataifishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Kifungu Namba 111 (i) ambayo inaruhusu kutaifisha mali itakayokutwa hifadhini.
Alisema kumekuwa na malalamiko juu ya utaratibu wa upigaji mnada mifugo iliyotaifishwa ikiwemo kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi, wenye mifugo kutoruhusiwa kuingia na idadi tofauti ya mifugo mnadani.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kijuu alishukuru ushirikiano alioupata kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo alioieleza ina mafanikio makubwa ikiwemo wanyamapori kuanza kurudi maeneo yao katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi.

No comments:

Powered by Blogger.