Header Ads

WAUNGA MKONO UDHIBITI WA RASILIMALI ZA NCHI

 MuroTv

Waunga mkono udhibiti wa raslimali za nchi

Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
BARAZA la Wazee la Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limewataka Watanzania kuweka itikadi za vyama vyao pembeni na kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kujenga Tanzania mpya.
Pia baraza hilo limempongeza Rais Magufuli kwa hatua anazochukua dhidi ya watumishi wa umma wanaotumia nafasi zao kujinufaisha jambo linalochelewesha mkakati wa kukuza uchumi wa nchi.
Katibu wa baraza hilo, Flovian Kapinga alisema hayo jana wakati wa kikao cha wazee na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji mjini Mbinga.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito na wa Mji wa Mbinga, Robert Mageni. Kapinga alisema hatua za Rais Dk Magufuli ni nzuri kwani zinakusudia kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kuharakisha maendeleo na zinawanufaisha Watanzania wote, kurudisha uwajibikaji, heshima na uadilifu sehemu ya kazi kwa watumishi badala ya kuwanufaisha watu wachache.
Alisema dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda, kuimarisha miundombinu nchini kama ujenzi wa reli kanda ya kusini kutoka Mtwara hadi Mbamba bay na ulinzi na usalama wa nchi ukanda wa Ziwa Nyasa, ni mambo mengi mazuri ambayo Watanzania lazima wajivunie na kuunga mkono badala ya kubeza.
Kwa mujibu wa Kapinga, tangu Rais Magufuli achaguliwe, yamefanyika mambo mengi ya msingi ambayo wananchi lazima wayatambue kwani katika miaka miwili, kumeshuhudiwa uboreshaji wa shughuli za kilimo kwa kutumia matrekta jambo ambalo ni muhimu ili kufikia uchumi wa viwanda.
Akizungumzia elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, Kapinga alisema mpango huo umepokelewa vizuri na Watanzania wote. Hata hivyo, wazee hao wamemwomba Rais mpango huo kufika hadi kidato cha sita ili kutoa fursa kwa watoto wanaotoka katika familia za watu maskini kufanikisha ndoto zao za kupata elimu ya juu.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuanza kwa Mradi wa Umemejua Vijijini (REA), mkombozi kwa viwanda vidogo, ujenzi wa kiwanda cha dawa za binadamu wilayani Bagamoyo na ujenzi wa reli mpya nchini. Alisema hayo ni msingi wa maendeleo ya taifa ambayo Watanzania lazima wajivunie rais wao

No comments:

Powered by Blogger.