TUME YA UTUMISHI YASIKILIZA RUFAA 48
MuroTv
Tume ya Utumishi yasikiliza rufaa 48
31 Mai 2017
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki
Katibu wa Tume hiyo, Nyakimura Muhoji alisema kati ya rufaa hizo, 32 zilikataliwa, 13 zilikubaliwa na mbili tume imeagiza mashtaka yaanze upya baada ya kubaini kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu na rufaa moja ilikataliwa kwa sababu ilikatwa nje ya muda uliotolewa kisheria.
Alisema waliokata rufaa hizo walikuwa na hatia ya kukiuka maadili ya kazi na taaluma zao, kutotekeleza majukumu ipasavyo, ubadhirifu, rushwa, wizi wa fedha na mali, udanganyifu wa vyeti, kudhalilisha utumishi wa umma, uzembe, kutoa taarifa za uongo na utovu wa nidhamu.
Alisema kosa la utoro kazini lilihusu watumishi wengi waliofukuzwa kazi na makosa hayo yalitendwa na watumishi katika makundi ikiwemo utumishi wa afya, utumishi wa serikali za mitaa na utumishi Serikali Kuu. Katibu huyo alisema malalamiko matatu yaliamriwa kati ya hayo mawili yamekubaliwa na moja limerejeshwa mamlaka husika ili lishughulikiwe.
Muhoji pia alizitaja changamoto walizokutana nazo kuwa ni usimamizi rasilimali watu katika utumishi wa umma ikiwemo mamlaka za nidhamu, kutowachukulia hatua kwa wakati au kutowachukulia hatua waliokosa.
Nyingine ni baadhi ya mamlaka za nidhamu kutounda kamati za uchunguzi au kutumia taarifa za uchunguzi wa awali kama zilivyowasilishwa kwao, upungufu katika uaandaaji wa mashitaka na uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu na waajiri na mamlaka za nidhamu kutoa uamuzi nje ya muda.
Alisema zipo hatua ambazo wamechukua kukabili changamoto hizo ikiwemo kutoa maelekezo ya kuboresha maeneo yenye upungufu kwa taasisi zilizokaguliwa, kuziandikia taasisi zenye hoja za ukaguzi ili zijibiwe.

No comments:
Post a Comment