Taarifa mpya kuhusu Usafiri wa treni Dar
Treni ya abiria kati ya Ubongo na Stesheni jijini Dar es Salaam
iliyopata ajali leo asubuhi eneo la Mabibo Magengeni baada ya mabehewa
matano kuacha njia, imeendelea na safari saa 10:00 jioni.
Mhandisi wa Mitambo wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Shija Isanga
amesema tatizo lililopo ni kuwa reli imechakaa, hivyo wataalamu wa
ujenzi walifanya kazi ya kukarabati mataruma kuhakikisha safari
zinarejea kama kawaida.
Awali, akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli,
Salum Kisaye alisema ajali hiyo haikuleta madhara kwa binadamu.
Ofisa Mawasiliano wa TRL, Midladjy Maez, amesema ajali hiyo ilitokea
leo (Ijumaa) saa 12:30 asubuhi treni hiyo ilipokuwa ikitokea Ubungo
Maziwa kuelekea Stesheni.
Amesema mabehewa ya nyuma yaliacha njia na kusababisha taharuki na
kwamba walihamishiwa mabehewa mengine na waliendelea na safari.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema walishtushwa na kishindo na kuona
vumbi ndipo walipoenda eneo la tukio na kukuta mabehewa yakiwa yameacha
njia yake.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Ismail Rajabu amesema tatizo
lililopo reli hiyo inatakiwa ifanyiwe ukarabati kwa kuwa sehemu nyingi
zina nyufa.
Amesema mataruma yaliyopo yanaonekana yamechakaa, hivyo aliiomba Serikali kusimamisha usafiri ili kujenga upya reli hiyo
No comments:
Post a Comment