ASALI YENYE MIAKA 2000 YAKUTWA KWENYE MAPIRAMIDI
MAPIRAMIDI ya Misri ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia lakini ndani yake, kumegunduliwa maajabu mengine yaliyowashangaza wengi.
Mwaka 2006, wataalamu wa mambo ya kale
waliokuwa wakifanya utafiti kwenye mapiramidi hayo, waligundua kitu
kilichowashangaza sana. Ndani ya moja ya mapiramidi hayo, walikuta
chungu kikubwa, kikiwa na asali.
Uchunguzi wao ulionesha kwamba asali
na chungu hicho, vimekaa eneo vilipokutwa kwa zaidi ya miaka 2000 lakini
cha ajabu, asali bado ilikuwa nzima na waliopata fursa ya kuionja,
walikiri kwamba ilikuwa na ladha halisi ya asali na usingeweza
kuitofautisha na asali iliyotoka kurinwa muda huo.
Jambo hilo liliwashangaza sana wote
waliokuwa kwenye utafiti huo ambapo ili kujiridhisha, ilibidi chungu
hicho kitolewe na kupelekwa maabara ambapo uchunguzi wa kina ulianza
kufanyika.
Kilichobainika, ni kwamba licha ya
asali hiyo kukaa miaka yote hiyo, bado haikupoteza sifa yake hata moja,
ilikuwa katika ubora wake na ingeweza kutumika kwa shughuli yoyote kama
yalivyo matumizi ya kawaida ya asali.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi kwenye
chungu hicho, ulibaini mabaki ya mifupa ya mtoto mdogo, yaliyokuwa chini
kabisa ya chungu, ambayo hayakuwa yamecha-nganyikana na asali hiyo.
Baadaye, ikaja kubainika kwamba watu
walioishi kwa kipindi hicho, walikuwa na utamaduni wa kuwatoa kafara
watoto wachanga, hasa wa kiume kwa kuwaua kisha kuiweka miili yao kwenye
vyungu vikubwa vilivyojaa asali, kama sadaka kwa miungu yao ili
kuwakinga na mabalaa mbalimbali.
Ili kujiridhisha zaidi, watafiti hao
walirudi tena kwenye mapiramidi ambapo walifanikiwa kupata vyungu
vingine kadhaa, vikiwa na asali ambayo chini ilikuwa na mabaki ya mifupa
ya watoto, lakini yenyewe ikiwa kwenye ubora wake uleule.
Kitaalamu, inaelezwa kwamba asali
ndiyo chakula pekee kisichoweza kuharibika. Hii ni kwa sababu, asali ina
mchanganyiko wa kipekee wa maji na virutubisho vingine, ambavyo kwa
pamoja hufanya kiwango cha asidi (pH) kuwa kati ya 3.2 hadi 4.5.
Kiwango hiki cha asidi, hakiwezi
kuruhusu kuzaliana au kuishi kwa kiumbe chochote, si bakteria, vimelea
vya magonjwa wala virusi ndiyo maana huwa haiharibiki hata ikae maelfu
ya miaka.
No comments:
Post a Comment