MRADI WA UHIFADHI NA MAENDELEO YA IKOLOJIA YA PORI LA AKIBA LA SELOUS (SECAD) ULIOFADHILIWA NA SERIKALI YA UJERUMANI
MuroTV
KIMATAIFA
PROF. JUMANNE MAGHEMBE AZINDUA MRADI WA UHIFADHI NA MAENDELEO YA IKOLOJIA YA PORI LA AKIBA LA SELOUS (SECAD) ULIOFADHILIWA NA SERIKALI YA UJERUMANI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijaribu
moja ya gari baada ya uzinduzi wa magari sita aina ya Land Cruiser
ambayo ni sehemu ya Mradi huo.
"Mradi huu ni muhimu sana kwakua utasaidia kuongeza nguvu
kwenye jitihada zetu za kuendeleza na kuimarisha hifadhi ya pori hili la
Selous ikiwemo upatikanaji wa vitendea kazi muhimu pamoja na
kutuongezea nguvu kwenye mapambano dhidi ya ujangili", alisema Prof.
Maghembe.
Alisema jitihada ambazo Serikali imeshazifanya katika pori
hilo ni pamoja na kuimarisha doria za ndege zenye rubani na zisizo na
rubani (drones), kutoa mafunzo ya jeshi usu kwa askari, kuongeza
maaskari pamoja na vitendea kazi ambapo katika mwaka ujao wa fedha
Serikali itatoa magari mengine 15 kusaidia pori hilo.
"Pamoja na jitihada hizo tunawekeza dola za kimarekani
Milioni 156 (sawa na Shilingi bilioni 349.441) kwa ajili ya kuboresha
pori hili (Selous), Ruaha, Mikumi, Rungwa na Kitulo kuhakikisha watalii
wanatembelea maeneo haya na kuondoa kile kikwazo cha wao kutotembelea
hifadhi za kusini, hiyo inaenda sambamba na kuimarishwa kwa shirika la
ndege la Serikali la Air Tanzania na kuondoa changamoto iliyokuwepo ya
usafiri wa anga", alisema Prof. Maghembe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa
kushirikiana na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke
amezindua Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la
Selous SECAD (Selous Ecosytem Conservation and Development Program)
ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali
ya Tanzania, mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, WWF (World
Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society).
Akizungumza katika hafla iliyofanyika jana, Matambwe na
Tagalala Selous, Mkoani Morogoro, Waziri Maghembe alisema Serikali ya
Ujerumani kupitia benki ya KFW imechangia Euro Mil. 18 (sawa na Shilingi
Bil. 45.124) katika mradi huo wa miaka mitano huku mashirika ya WWF
(World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society) yakichangia
Euro laki 4 kila moja (sawa na Shilingi bil. 2.005) katika mradi huo.
Pamoja na uzinduzi huo alizindua pia Mpango Kazi wa Dharura wa
kuendeleza pori hilo.
Magari sita aina ya Land Cruiser yaliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kama sehemu ya mradi wa SECAD.
Akizungumzia changamoto ya ujangili katika pori hilo
alisema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo hilo
ambapo majangili wengi wameshakamatwa katika maeneo ya Tunduru, Namtumbo
na maeneo ya katikati ya Selous. Alisema changamoto hiyo bado ipo
katika maeneo ya Mkoa wa Ruvuma ambapo imeripotiwa na kamati ya ulinzi
na usalama ya Mkoa huo kuwa kuna upatikanaji wa silaha za kivita kutoka
nchini Msumbiji ambazo zinapatikana kwa watu kubadilishana na magunia ya
mchele changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
Wakati huo huo, Prof. Maghembe akijibu swali aliloulizwa
na wanahabari kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya kauli aliyoitoa bungeni
hivi karibuni ikiwa na dhamira ya kuunganisha taasisi zote za uhifadhi
nchini alisema, tayari ameshaunda kamati ya watu sita ikiongozwa na Mkuu
wa Chuo cha Wanyamapori Mweka, Prof. Japhary Kidegesho kwa ajili
kuangalia namna bora ya kutekeleza azma hiyo. "Tayari kamati hiyo
imeshaanza kazi na itaonana na wadau mbalimbali kupata maoni yao na
katika kipindi cha mwezi na nusu watatuletea ripoti", alisema.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
(kushoto) na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke wakikata
utepe kuashiria uzinduzi wa magari sita aina ya Land Cruiser ambayo ni
sehemu ya Mradi aliouzindua wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori
la Akiba la Selous (SECAD).
NA HAMZA TEMBA – WMU
Kwa upande wake Balozi Konchanke alimuahakikishia Prof.
Maghembe kuwa Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali
ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili
hifadhi hiyo ikiwemo ubovu wa miundombinu na uvamizi pori hilo kwa
faida ya jamii kwa ujumla. Aidha, alitoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi
wa Wanyamapori Tanzania TAWA kubuni mbinu mpya za kukabiliana na
changamoto zilizopo.
Meja Jenerali Gaudence Milanzi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, alisema "Serikali kwa kushirikiana na wadau wa
uhifadhi imefanya kazi kubwa kuhakikisha Selous haiondolewi katika
orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyopo hatarini kutoweka, hiyo ni
pamoja na kunzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyanapori Tanzania
TAWA, kuanzishwa kwa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ujangili na
miradi mbali ikiwemo huu wa SECAD uliozinduliwa leo ambayo kwa kiasi
kikubwa imeasaidia katika kuendesha hifadhi zetu pamoja na kusaidia
kwenye mapambano dhidi ya ujangili".
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania, TAWA, Martin Loibooki aliishukuru Serikali ya
Ujerumani kwa mradi huo na kusema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa
kukabiliana na changamoto mbalimbali katika pori hilo ikiwemo ya uhaba
wa vitendea kazi, miundombinu ya barabara na ujangili na hivyo kuifanya
hifadhi hiyo iendelee kuwa miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia.
Pori la Akiba la Selous ni hifadhi kubwa kuliko zote
Tanzania ikiwa ukubwa wa Kilomita za mraba 50,000. Hifadhi hiyo ambayo
ipo katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ina vivutio
vingi vya utalii huku ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
miundombinu ya barabara, ujangili, rasilimali watu na vitendea kazi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
(katikati) akipokelewa jana katika uwanja mdogo wa ndege wa Matembwe
uliopo Selous na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Loibooki (wa pili kushoto)
alipowasili kwa ajili ya hafla hiyo. Nyuma yake anayeshuka kwenye ndege
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kushoto).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana katika kituo cha
Tagalala, ndani ya Pori la Akiba la Selous Mkoani Morogoro.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke akizungumza katika hafla hiyo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika hafla hiyo jana.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Prof. Faustin Kamuzora akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu, Hamis Semfuko akizungumza katika
hafla hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Martin Loibooki akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika jana, Tagalala, Selous.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
(kulia) akizindua Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo wa Ikolojia ya Pori la
Akiba la Selous (SECAD) ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa
ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika hafla iliyofanyika jana
Matambwe, Selous Mkoani Morogoro. Wanaoshudia kulia kwake ni Balozi wa
Ujerumani, Egon Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof.
Faustin Kamuzora.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
(kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo,
Prof. Alexander Songorwa Mpango Kazi wa Dharura wa Kuendeleza Pori la
Akiba la Selous baada ya kuuzindua sambamba na mradi wa Uhifadhi na
Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD). Kulia kwake ni
Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof.
Faustin Kamuzora, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania, Martin Loibooki na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu
wa TANAPA, Dkt. Dembe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Prof. Faustin Kamuzora (katikati) na
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA), Meja Jenerali Mstaafu, Hamisi Semfuko (kulia).
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Mghembe (wa tatu kushoto), Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke
(wa pili kushoto) na viongozi wengine wakuu wa Wizara na Taasisi pamoja
na washiriki wa hafla hiyo. Nyuma yao ni ziwa Tagalala ambalo ni sehemu
ya kivutio cha utalii ndani ya hifadhi hiyo.
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba la Selous wakiwa katika hafla hiyo.
Muro Tv Ipo Play Store…Download HAPA ,Tuwe tunakutumia habari kwa haraka zaidi,kwa mawasiliano zaidi wasiliana nasi kwa namba:0768786851, whatsapp:0768786851

No comments:
Post a Comment