Header Ads

LESOTHO WAINGIA RADA ZA MAYANGA

MuroTv

Lesotho waingia rada za Mayanga

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga
KOCHA wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Salum Mayanga amesema tayari amepata mbinu za wapinzani wao hivyo wanakwenda kambini Misri kwa tahadhari.
Mayanga na kikosi cha wachezaji 21 wa Stars waliondoka nchini jana jioni kuelekea Cairo, Misri kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Lesotho utakaochezwa Juni 10, mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya kuelekea Misri, Mayanga alisema watakuwa wanafanya mazoezi kwa tahadhari wakijiandaa kiufundi na kimbinu kuwakabili wapinzani wao. “Tumewaona Lesotho ni wazuri, wamekuwa wakishambulia kwa pamoja na kuzuia kwa pamoja.
Pia ni timu inayojua kumiliki mpira,” alisema. Aliongeza kuwa alifuatilia wapinzani wake hao kupitia mechi za mwaka jana ambapo wanaonyesha kupata matokeo mazuri. Alizungumzia sababu za kuchagua Misri kwa ajili ya kambi hiyo kwamba kuna hali ya hewa nzuri inayofanana na Dar es Salaam na vile vile kuna miundombinu bora kwa ajili ya mazoezi.
Mayanga alitaja sababu za kuwaacha wachezaji wawili Mwinyi Haji wa Yanga na Aggrey Morris wa Azam na nafasi zao kuchukuliwa na Gadiel Michael wa Azam na Nurdin Chona wa Tanzania Prisons ni kutokana na mkanganyiko wa sheria na kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya Zanzibar kuwa wanachama kamili wa Shirikisho hilo.
Alisema bado kuna hofu kwa jamii juu ya wachezaji wa Zanzibar na Tanzania bara, hivyo ameona awaache kwanza mpaka jamii itakapoelimishwa sheria na kanuni na nani anayehitaji kuchezeshwa. Waliokwenda kambini Misri ni makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael. Walinzi wa kati Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shiza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).

No comments:

Powered by Blogger.