Header Ads

HOTELI MPYA YA KIMATAIFA YAJA MJI MKONGWE

Hoteli mpya ya kimataifa yaja Mji Mkongwe

Mkurugenzi wa Kampuni ya Pennyroyal Gibraltar, Saleh Mohamed Said akibadilishana hati ya makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa hoteli ya kitalii visiwani Zanzibar na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Alex Kyriakidis wa Kampuni ya Kimataifa ya Marriott katika hafla iliyofanyika hivi karibuni Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). (PIcha kwa hisani ya Pennroyal).
 
TAASISI ya Kimataifa ya Marriott International ikishirikiana na Pennyroyal Gibraltar Limited, zimesaini makubaliano ya kuzindua aina mpya ya hoteli ya kimataifa, Ritz- Carlton kivutio kikubwa Zanzibar kwa mwonekano.
Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Marriott International Mashariki ya Kati na Afrika, Alex Kyriakidis alisema hoteli hiyo kubwa ya kifahari itazinduliwa mwaka 2021 na itakuwa na vyumba 90 vyenye kila kitu cha muhimu.
Kyriakidis alisema jana kuwa Ritz-Carlton itakuwa umbali wa dakika 45 kwa gari kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Karume, Zanzibar. Katika taarifa yake, alisema pamoja na kuwa kivutio kwa wengi, kuonesha mandhari halisi ya Zanzibar kwa wageni kutoka nje, itakuwa rahisi kwa anayepata huduma kulifikia eneo maarufu la malikale, Mji Mkongwe lililohifadhiwa chini ya Shirika la Kimataifa la Sayansi na Elimu (UNESCO).
“Kwa kuwa na aina hiyo ya hoteli itakayochukua hekta 1750 Kaskazini Mashariki mwa Ukanda wa Bahari ya Hindi, Zanzibar itakuwa na nafasi nzuri ya kushindana na Mauritius, Shelisheli na Maldives,” alisema.
Wakurugenzi wa Pennyroyal Gibraltar, Saleh Said na Brian Thomson walisema kwa nyakati tofauti wamefurahishwa kushirikiana na Marriott International kuzindua hoteli hiyo na kwamba watahakikisha inakuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Pamoja na kuwa na huduma zote muhimu zinazohitajiwa na watu muhimu watakaofika katika hoteli hiyo ikiwemo vifaa vya burudani, bwawa la nje la kuogelea, mahali maalumu watoto kuburudika katika fukwe, kutakuwa pia na eneo maalumu kwa ajili ya kutolea huduma za afya katika fukwe.

No comments:

Powered by Blogger.