DARUSO WAMUUNGA MKONO MAGUFULI MCHANGA WA DHAHABU
MuroTv
Daruso wamuunga mkono Magufuli mchanga wa dhahabu
30 Mai 2017Rais wa Daruso, John Jeremiah alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la serikali yao juu ya ripoti ya Tume ya kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena ya mchanga (makinikia).
Jeremiah alisema ni imani ya Watanzania wengi kuona juhudi za Rais Magufuli kuhusu nidhamu na uwajibikaji zinazoleta uhuru wa kiuchumi, zikiungwa mkono na kutekelezwa na kila mwenye dhamana ya uongozi.
“Ili kukuza uchumi, jitihada zinahitajika kwa viongozi wenye dhamana kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia maadili wakitambua utendaji wao utapimwa hadi vizazi vijavyo na kuenzi waasisi wa nchi,” alisema.
Alisema jitihada za Rais Magufuli zinafaa kuungwa mkono, hivyo Daruso inawaomba marais wengine wa Afrika kuiga anachofanya Rais Magufuli. Alisema Daruso inawathibitishia Watanzania na Rais Magufuli kuwa wako naye bega kwa bega katika harakati zake za kuikomboa nchi kiuchumi.
Kuhusu ripoti ya mchanga, alisema Daruso inashauri kuwa fedha zote zilizotokana na mchanga uliopelekwa nje ya nchi kwa miaka 19, zikokotolewe na kampuni iliyokuwa ikihusika kufanya hivyo iwalipe Watanzania na kulipa kodi kiwango kinachostahili na ishitakiwe.
Alisema katika suala hilo, wanasheria waliopo nchini watumike vyema kuishauri serikali ili shauri kama hilo liweze kuwa lenye manufaa nchini, huku mikataba yote ya madini ikiangaliwa upya ili pande zote zinufaike.
Alisema viongozi wenye dhamana ya kutetea wananchi walioshindwa kutumia nafasi hizo kimkakati na kiuongozi na kulisababishia hasara kubwa taifa wachunguzwe na wakibainika wamekosa, wafilisiwe na kufungwa.
Alisema mikataba na kampuni hizo za madini lazima iruhusu ukaguzi wa mara kwa mara migodini kwa maofisa wa serikali na wataalam wa ndani ya nchi na vipengele vioneshe kuwa wako tayari kukaguliwa mahesabu yao ya kifedha na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

No comments:
Post a Comment