Waangalizi: Uchaguzi wa Kenya ulikuwa wa haki
![]() |
| Kiongozi wa waangalizi wa uchgauzi kutoka mataifa ya Jumuiya ya Madola aliyekuwa rais wa Ghana John Mahama |
Waangalizi wa
uchaguzi kutoka mataifa ya kigeni wamesema wana matumaini na shughuli ya
uchaguzi nchini Kenya licha ya madai ya upinzani kuhusu udanganyifu
mkubwa.
''Uchaguzi wa Jumanne ulikuwa wa haki'', wamesema waangalizi wa Muungano wa Afrika na wale wa mataifa ya jumuiya ya madola.Muungano wa Ulaya umesema kuwa wagombea ni sharti kukubali matokeo kwamba kushindwa ni jambo la kawaida katika shindano la kidemokrasia.
Mgombea wa upinzani Raila Odinga amedai kwamba hesabu ya kura iliingiliwa ili kumpatia ushindi rais aliyepo madarakani Uhuru kenyatta.
Siku ya Jumatano, alisema kuwa mfumo wa kutangaza matokeo wa IEBC ulikuwa umedukuliwa na kwamba Kenya ilikuwa ikishuhudia wizi mkubwa ambao haujaonekana katika historia ya taifa hilo.
IEBC inasema kuwa kulikuwa na jaribio la kuudukua mfumo wake , lakini likafeli.
Kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi katika Jumuiya ya madola na aliyekuwa rais wa Ghana John Mahama amesema kuwa hakuna sababu ya kutilia shaka uwezo wa tume hiyo kuandaa uchaguzi wa huru na haki.
''Tunaamini kwamba uchaguzi ulifanyika katika njia ya uwazi na ya haki na kwamba Wakenya ni lazima wapongezwe kwa uchaguzi huo'',aliongezea katika mkutano na vyombo vya habari mjini Nairobi.
Akitoa maoni kama hayo, kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Afrika na ambaye alikuwa rais wa Afrika Kusini Thambo Mbeki alisema kuwa ameridhishwa na vile tume hiyo ya uchaguzi ilivyoandaa uchaguzi huo.
![]() |
| Kiongozi wa waangalizi wa ujumbe wa Umoja wa Afrika Thabo mbeki |
Akiongoza kundi la waangalizi wa kituo cha Carter, aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry alisema kuwa uadilifu wa shughuli yote ya uchaguzi ulikuwa mzuri.
Amezitaka pande zote mbili kusubiri matokeo ya mwisho na walioshindwa kukubali matokeo.
Katika taarifa ,waangalizi wa muungano wa Ulaya walisema kuwa upinzani uliwasilisha madai yanayofaa kutiliwa ''maanani'' na kwamba ulikuwa wajibu wa IEBC kukamilisha hatua zilizosalia kwa njia ya uwazi na kuheshimu sheria.
''Wagombea na wafuasi wao ni lazima wakubali kwamba kutoshinda ni swala la kawaida katika shindano la kidemokrasia'', alisema Kiongozi wa EU Marietje Schaake.
''Udanganyifu wowote ama changamoto kuhusu uchaguzi huo na matokeo yake ni lazima kutatuliwa kupitia mahakama'', aliongezea.
Tume ya IEBC imesema kuwa inatumai kutoa matokeo yote ya urais siku ya Ijumaa.
![]() |
| Waangalizi wa uchaguzi kutoka kituo cha Carter Centre wakiongozwa na aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni wa Marekani John Kerry |
Madai ya bwana Odinga ya wizi wa kura yalisababisha kuzuka kwa ghasia siku ya Jumatano, lakini polisi wamekana madai kwamba watu wawili waliuawa katika ghasia hizo za uchaguzi.




No comments:
Post a Comment