ACACIA kutafuta nafuu Marekani yatangaza kufungua kesi.
Baada ya Serikali ya Tanzania kuweka zuio la kutosafirisha Makinikia Kampuni ya Acacia, jana ilitangaza kufungua ‘kesi’ ya kuomba upatanishi wa mgogoro unaoendelea baina yake na serikali.
Taarifa iliyotolewa jana na Acacia ilisema kampuni hiyo imewasilisha taarifa hiyo ya kutafuta upatanishi kwa niaba ya kampuni zake tanzu za Bulyanhulu Gold Mine Limited (BGML) na Pangea Minerals Limited (PML), inayomiliki mgodi wa Buzwagi.
Kampuni hiyo ya Uingereza inamiliki pia mgodi wa dhahabu wa North Mara, lakini ni miwili hiyo ambayo mali yake huhusisha uchenjuaji wa makinikia.
Migogoro ya kimataifa ya kiuwekezaji hutatuliwa na ama Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) au Chemba ya Kimataifa ya Biashara (ICC).
Ingawa taarifa ya Acacia haikueleza imefungua wapi ombi lake la kutaka upatanishi wa mgogoro wa makinikia, chanzo cha kuaminika kiliiambia pande hizo mbili zitaketishwa pamoja ICSID yenye makao yake makuu Washington DC, Marekani.
“Taarifa za kusudio hili zinahusu mgogoro wa sasa kati ya Serikali ya Tanzania na kila moja kati ya BGML na PML kusuluhishwa,” ilisema Acacia katika taarifa yake iliyowekwa kwenye tovuti yake na kuongeza:
“Hii ni kuendana na mchakato wa utatuzi wa migogoro uliokubaliwa na Serikali ya Tanzania katika Makubaliano ya Uendelezaji Madini na BGML and PML.
“Uwasilishaji wa taarifa ya kutafuta upatanishi kwa wakati huu ni muhimu kwa ajili ya kuilinda kampuni. Pamoja na hatua hii, Acacia bado ina mtazamo kuwa mazungumzo nje ya vyombo rasmi ndiyo njia bora ya utatuzi wa migogoro iliyopo na kampuni itaendelea kufanya jitihada kufanikisha hili.”
Acacia ilisema serikali pia imeiarifu Barrick, kampuni yake mama, kuwa kwa sasa ingependa kuendelea na mazungumzo yao, hivyo, “Acacia haitashiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo yatakapoanza.”
“Suluhusho lolote litakaloweza kubainishwa kutokana na mazungumzo hayo litalazimika kupitishwa na Acacia, na kampuni itashirikiana na Barrick kwa hali na mali kusapoti mazungumzo hayo.
KULIPA FEDHA
Juni 14, Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ya Canada ambayo ni mmiliki mkubwa wa Acacia, Prof. John Thornton alifanya mazungumzo na Rais John Magufuli na kukubali kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na udanganyifu ambao umegundulika kwenye biashara ya makinikia nchini.
Juni 14, Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ya Canada ambayo ni mmiliki mkubwa wa Acacia, Prof. John Thornton alifanya mazungumzo na Rais John Magufuli na kukubali kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na udanganyifu ambao umegundulika kwenye biashara ya makinikia nchini.
Mazungumzo hayo yalifanyika ikiwa zimepita siku tatu tangu Rais akabidhiwe ripoti ya kamati maalum ya pili iliyochunguza masuala ya sheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi.
Ripoti iliyowasilishwa na mwenyekiti Prof. Nehemia Osoro, ilisema nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.
Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.
Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.
Taarifa ya Ikulu ilisema baada ya mazungumzo hayo, Prof. Thornton alisema kuwa kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na kwamba ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Acacia imejikuta katika wakati mgumu baada ya kamati ya kwanza iliyoteuliwa na Rais Magufuli Machi 29, ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini, kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena yenye makinikia kuonyesha kuwapo kwa udanganyifu.
Acacia ndiyo msafirishaji mkuu wa makinikia nchini.
Kamati hiyo maalumu ilikuwa chini ya uenyekiti wa Profesa wa masuala ya miamba, Abdulkarim Mruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Baada ya kamati ya kwanza kumkabidhi ripoti ya uchunguzi Mei 24, Rais Magufuli alichukua uamuzi wa kusitisha upelekaji mchanga nje ya nchi mpaka itakapoelezwa vinginevyo baadaye.
Na baada ya Kamati ya pili ya Rais kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia yanayosafirishwa nje ya nchi tangu mwaka 1998 kugundua Acacia haijasajiliwa kwa mujibu wa sheria, Rais Magufuli alisitisha moja kwa moja usafirishaji huo.
Akizungumzia Acacia kukosa usajili, Rais Magufuli aliwashangaa viongozi walioiacha ifanye bishara za ma-trilioni ya shilingi.
“Tujiulize sisi viongozi ni mara ngapi Watanzania wenzetu wasiposajiliwa tunawashughulikia kwa mitutu ya bunduki?” Aliuliza Rais kwa masikitiko.
“Tujiulize sisi viongozi ni mara ngapi Watanzania wenzetu wasiposajiliwa tunawashughulikia kwa mitutu ya bunduki?” Aliuliza Rais kwa masikitiko.
“Mmachinga akienda bila kusajiliwa anafukuzwa kwenye maeneo yao, mara ngapi wafanyabiashara wadogowadogo wasio na leseni wanashughulikiwa?
“Huyu tumemuacha tangu mwaka 1998 hadi sasa.
“Tuna wanasheria wengi na wengine wanatisha utashtakiwa. Mali ni yangu, nimeamua kuiangalia mwenyewe halafu unishtaki uendelee kuchimba? Kukulinda nakulinda mimi, napeleka polisi wanalinda migodi yote, halafu unishtaki na uendelee kuchimba?
“Kwa kisingizio kwamba umetengeneza ajira, nikiruhusu watu si nitatengeneza ajira mamilioni? Tatizo litakuwa wangapi watakufa wakigombea dhahabu.
“Tumechezewa vya kutosha, haiwezekani tukawa sisi ndiyo wa kuibiwa tu.”
No comments:
Post a Comment