Header Ads

MREMA ATAKA MAGUFULI AUNGWE MKONO USIMAMIAJI RASILIMALI

MuroTv

Mrema ataka Magufuli aungwe mkono usimamiaji rasilimali

MWENYEKITI wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema
MWANASIASA mkongwe nchini, Augustine Lyatonga Mrema ametoa mwito kwa wananchi kuziunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kusimamia rasilimali za nchi kwa kuwa hiyo ni miongoni mwa ahadi zake katika Uchaguzi Mkuu ambazo ziliwavutia kumchagua.
Mrema amesema nia ya Rais ni nzuri na anachofanya, kama alivyoahidi mwenyewe katika kampeni za uchaguzi, ni kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya nchi na kuiondoa Tanzania katika kuwa ombaomba wakati ina utajiri wa kutosha.
Rais amekuwa akisema Tanzania haipaswi kuwa ombaomba badala yake, yenyewe ndiyo inatakiwa itoe misaada kwa nchi nyingine. Akizungumza nyumbani kwake jana kuhusu hatua ya Rais kuzuia mchanga wa dhahabu (makinikia) kusafirishwa nje kuchenjuliwa, Mrema alipongeza hatua ya Rais na kusema Watanzania wanapaswa kuungana naye kwa kuwa anafanya jambo zuri kwa manufaa ya maendeleo ya Watanzania wote.
“Rais anaishi kwa maneno yake, amekuwa mtu wa vitendo, aliahidi wakati wa kampeni kusimamia rasilimali za nchi yetu ili zitumike kwa manufaa yetu sote na sisi tukamchagua hivyo hatuna budi kuendelea kumuunga mkono bila ya kusita,” alisema mbunge huyo mstaafu wa upinzani.
Mrema alisema huko nyuma pamoja na wananchi kupiga kelele kuhusu utoroshwaji wa rasilimali, hakukuwa na mkakati wa kitaifa unaosimamiwa kwa dhati na Rais lakini sasa Watanzania wamepata Rais mwema, mwadilifu na mcha Mungu anayetetea rasilimali za taifa kwa nguvu zake zote.
“Tutaishi katika hali hii ya kuogopa kutetea cha kwetu mpaka lini? Wito wangu kwa Watanzania wote kwa umoja wetu, hakuna Rais aliyethubutu kushughulikia jambo hili, hivyo tumuunge mkono kwa hatua hii kubwa na ya kikistoria aliyoichukua,” alisisitiza Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.
Naye mwanazuoni mwandamizi na mchambuzi wa masuala ya jamii, Dk Charles Kitima katika mahojiano maalumu amempongeza Dk Magufuli kwa dhamira yake ya kulinda rasilimali za nchi. Dk Kitima alisema licha ya baadhi ya watu kubeza takwimu za ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza suala la madini, binafsi anaiunga mkono na kuwataka wananchi kuiamini taarifa hiyo kwani imetokana na wataalam wazalendo waliofanya kazi hiyo kwa maslahi mapana ya nchi.

No comments:

Powered by Blogger.