TETEMEKO LA ARDHI LAUA, POLISI AKIHOJI MTUHUMIWA MWANZA
Tetemeko la ardhi laua, Polisi akihoji mtuhumiwa Mwanza
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
Imeandikwa na Prosper Muro
Imechapishwa: 26 Mai 2017
TETEMEKO lingine limetokea katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na
kusababisha kifo cha Polisi aliyekuwa akimhoji mtuhumiwa Mwanza.
Tetemeko la jana limetokea takribani miezi tisa baada ya Septemba mwaka
jana kusababisha vifo kadhaa na uharibifu wa mali pia mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo jana walithibitisha kuwapo
kwa tetemeko hilo na kifo cha Polisi wa kike mkoani Mwanza. Kamanda
Msangi alimtaja askari aliyekufa kwa mshituko kuwa ni mwenye namba za
kijeshi, WP 4674, Koplo Joyce wa Kituo cha Polisi cha Misungwi.
“Tukio hili limetokea mchana majira ya saa saba; walikuwa ofisini
wanahoji mtuhumiwa basi akapata mshituko… wakati wanatoka nje, akafariki
maana huwa ana matatizo ya moyo,” alieleza Kamanda Msangi. Kamanda
Mponjoli alisema tetemeko hilo lililodumu kwa dakika mbili hivi,
limepita karibu wilaya zote za Mkoa wa Geita, Chato, Geita, Bukombe na
Mbogwe.
“Hata hivyo katika ukanda wote, huu hatujapata taarifa za madhara
ingawa bado tunafuatilia zaidi,” alisema Kamanda Mponjoli. “Hili
tetemeko lilikuwa na kishindo kikubwa kama ngurumo za radi au kitu
kinacholipuka na tulikuwa ofisini tukadhani ni mlipuko wa baruti za
kwenye mgodi wa GGM ingawa haukuwa mlipuko wa kawaida tuliouzoea,”
alisema.
Alisema kwa kuwa lilitokea mchana wakati wa kazi, watu walipata
kihoro na kukimbia. “Inaonekana kuna hali kama hiyo maana hata usiku wa
kuamkia leo (jana) yapata saa mbili hivi usiku, hali kama hiyo
ilijitokeza ingawa licha ya kuwa na nguvu, watu hawakujali sana,”
alisema Kamanda.
No comments:
Post a Comment