Header Ads

DEWJI ATIA NENO AJALI YA SHABIKI SIMBA

 MuroTv

Dewji atia neno ajali ya shabiki Simba

Katibu Mkuu wa zamani wa Klabu ya Soka ya Simba, Kassim Dewji
KATIBU Mkuu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji amezungumzia ajali iliyowapata mashabiki wa timu hiyo, Dumila, Morogoro juzi kuwa inamkumbusha ajali iliyotokea eneo hilo na kuondoa uhai wa viongozi wa Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Juzi gari aina ya Toyota Land Cruiser VX 8 yenye namba za usajili T 834 BLZ ilipata ajali eneo hilo na kumuua mwanachama mmoja wa Simba, Shose ‘Wazza’ Fidelis. Gari hilo lilikuwa na abiria sita akiwemo nahodha wa Simba, Jonas Mkude waliokuwa wakitoka Dodoma kushuhudia mechi ya fainali ya kombe la FA ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mbao Fc ya Mwanza uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mkude alipata majeraha kiasi shingoni ambapo alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alilazwa kwa matibabu kabla ya kuruhusiwa jana. Dewji, maarufu kama KD alisema jana, akiwa Katibu Mkuu wa Simba, anakumbuka kutokea ajali nyingine ya gari kama ya juzi katika eneo hilo la Dumila na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wao, Juma Salum na Mweka Hazina Mohamed Mwinyi.
“Nakumbuka tulikuwa tunatoka Dodoma kusuluhishwa mgogoro wetu, ndipo wakati tunarudi gari alilopanda Mwenyekiti na Mweka Hazina liligongwa na lori na viongozi wetu wale wakafariki,” alisema kiongozi huyo mwandamizi wa wana Msimbazi.
Wakati Mwenyekiti huyo anafariki, Simba ilikuwa kwenye mgogoro wa kubadili kadi zake za uanachama, wakati huo, marehemu Salum akitaka ziendelee kadi za zamani na upande wa kina Dewji aliyetokea kundi la Friends of Simba ukitaka zitumike mpya. Eneo hilo ndio pia alipopata ajali Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine wakati akitokea Dodoma pia kwenye kikao cha Bunge mwaka 1984.
Inaelezwa, katika eneo hilo, ajali za mara kwa mara zimekuwa zikitokea kiasi kwamba wakazi wa eneo hilo waliamua kujenga kanisa ili zifanyike ibada kwa imani zitasaidia waumini kukemea mapepo yanayosadikiwa kuchangia kutokea kwa ajali kila mara.
Hata hivyo, wataalam wa masuala ya barabara wamekuwa wakieleza nadharia tofauti kuhusu chanzo cha ajali zinazotokea katika eneo hilo wakidai zinatokana na madereva kujisahau na kusinzia kwa kuwa barabara imenyooka eneo kubwa bila kona au matuta.
Dewji alisema, akiwa kiongozi wa zamani wa Simba, amesikitishwa na kifo cha Shose kwani alikuwa mwanachama aliyekuwa akiambatana na timu mara kwa mara na kwa mazingira ya mechi yenye ushindani mkali juzi, kifo chake kitabaki kuwa cha shujaa.
“Huyo shabiki wetu ni shujaa, alikwenda kupambana kuhamasisha ushindi wa timu yetu. Kama mlivyoona, timu yetu imetwaa ubingwa wa FA na mechi mliona ilivyokuwa hivyo tumempoteza shujaa. Kazi ya Mungu haina makosa,” alisema.
Akizungumzia ubingwa huo utakaowawezesha Simba kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya miaka minne, Dewji alisema ni mafanikio makubwa kupata nafasi hiyo kwani walishadharaulika kwa kushika nafasi ya tatu na ya nne.
“Tulikuwa tunachukuliwa sisi ni wa kumaliza ligi kuanzia nafasi ya tatu au ya nne, maana nafasi ya kwanza na ya pili walikuwa wanapokezana Yanga na Azam. Ubingwa huu ni faraja na hatua nzuri kwa uongozi wa Rais Evans Aveva ambaye tangu achukue madaraka, hajashinda kikombe chochote.
Nampongeza, ni hatua nzuri,” alisema Dewji. “Mashindano haya ndio ya kujijenga na kujipanga vizuri. Nilipochukua madaraka Simba, mashindano yangu ya kwanza kushiriki yalikuwa haya.
Hapa ni kujenga timu kwani wachezaji wengi wamecheza ligi tu, huu ni wakati wao kujijenga kupitia mashindano haya baadaye wafanye vizuri na kushiriki Ligi ya Mabingwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Morogoro inamshikilia dereva Ahmed Kassim (35) mkazi wa Ilala, Dar es Salaam kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Shose na kusababisha abiria wengine wanne akiwemo Mkude, kujeruhiwa katika ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema jana ajali hiyo ilitokea juzi saa tano asubuhi baada ya dereva huyo kudaiwa kuendesha gari kwa mwendo kasi na baadaye gurudumu moja la gari hilo kupasuka na kisha gari lake kupoteza mwelekeo na kuacha njia na kwenda kuparamia kisiki cha mti na kugonga.
Kamanda aliwataja majeruhi wengine wanne kati ya abiria sita waliokuwa kwenye gari hiyo kuwa ni Mkude (26), mchezaji wa Simba na mkazi wa Manzese, Dar es Salaam ambaye alipatiwa matibabu na kuendelea na safari kurejea Dar es Salaam.
Aliwataja pia majeruhi wengine watatu waliokimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kupatiwa matibabu zaidi kuwa ni Jasmini Mdoe (24), Hamza Mpande (26) na Faudhia Ramadhan (25) wote wakazi za Manzese, jijini Dar es Salaam.
Ukiondoa ajali iliyowaua Mwenyekiti Salum na Mweka Hazina Mwinyi, hii ni mara ya pili kwa mashabiki wa Simba kupata ajali katika barabara ya Dodoma-Morogoro. Msimu uliopita mashabiki wa ‘Simba Ukawa’ walipata ajali wakiwa kwenye basi dogo wakienda Shinyanga kwenye mchezo wa timu yao na Stand United.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Makunganya ambapo pia baadhi ya mashabiki walifariki. Katika ligi ya msimu huu wa 2016,2017, Simba pia ilipoteza mashabiki wake wengine Tunduru, mkoani Ruvuma mwanzoni mwa mwaka huu waliofikwa na umauti katika msongamano wa kuipokea timu yao ilipokuwa ikienda Songea kucheza na Majimaji.
Mwezi uliopita, Simba pia ilipoteza shabiki mmoja Ifakara mkoani Morogoro aliyefikwa na umauti akishangilia bao la tatu la Muzamir Yassin katika mechi dhidi ya Mbao kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ambapo Simba ilishinda mabao 3-2.
Februari 25 mwaka huu shabiki wa Simba aliyekuwa mhasibu wa hoteli ya Courtyard alipata mshtuko na kufariki baada ya bao la Shiza Kichuya katika mechi ambayo walishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga.

No comments:

Powered by Blogger.