CCM YAOMBA WANANCHI WAMUUNGE MKONO MAGUFULI VITA YA UCHUMI
Muro Tv
CCM yaomba wananchi wamuunge mkono Magufuli vita ya uchumi
Katibu wa Sekretarieti, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaomba Watanzania wote kumuunga mkono
Rais John Magufuli kutetea maslahi ya nchi ikiwa ni pamoja na kuunga
mkono hatua ya kudhibiti rasilimali za madini ya dhahabu nchini.
Katibu wa Sekretarieti, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
(pichani) alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia
hatua ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospter Muhongo kwa madai ya kushindwa kusimamia sekta ya madini
nchini. Polepole aliwaomba Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli
kwani ni moja ya jambo litakalozidi kumuweka imara na madhubuti zaidi
kikazi.
Rais Magufuli alimtimua waziri baada ya kupokea ripoti ya Kamati
Maalumu iliyochunguza kilichomo katika kontena 277 zilizokuwa na
makinikia ambapo ilibainika kuwepo upotevu wa dhahabu ya sh trilioni
1.4. Katika ripoti hiyo ilibainika kuwepo kwa takwimu za uongo jambo
ambalo liliikosesha serikali mabilioni ya fedha kwa miaka 19 tangu
biashara hiyo ya kusafirisha nje ya nchi makinikia maarufu kwa mchanga
wa dhahabu ianze.
“Kazi kubwa ya CCM ni kuwa bora leo kuliko jana, tumedhulumiwa sana
mali tulizorithi, ipo haja na kizazi cha sasa kirithishe kwa kizazi
kijacho,” alisema Polepole. Alisema haki itabaki kuwa haki na awamu ya
tano ya uongozi inajinasibu ili rasilimali zitumike kwa upana na kila
Mtanzania. Alisema haiingii akilini mchanganuo wa kifedha wa thamani ya
mchanga huo umekuwa hivyo wakati awali ikitolewa viwango tofauti
visivyostahili jambo linalooonesha wametumia ujinga wa Watanzania
kuchuma mali.
“Hawa ni maharamia wa kiuchumi, walijaribu kuhonga sh bilioni 300
kabla ya ripoti kutolewa lakini Rais Magufuli aliwakatalia na kuwataka
wasubiri uchunguzi ukamilike,” alisema Polepole. Alisema CCM mpya ni
chachu ya maendeleo hivyo ni vyema kusimama pande zote kumpa moyo
kiongozi huo kwa kuwa jambo hilo ni la kipekee.
No comments:
Post a Comment