CCM YAVALIA NJUGA UHALIFU KIBITI
Muro Tv
CCM yavalia njuga uhalifu Kibiti
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uhalifu unaoendelea kutokea wilaya
za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani unatosha na kuitaka vyombo
vya ulinzi na usalama kulichukulia suala hilo kwa uzito likome.
Kimesema yeyote mwenye dhamana na suala hilo ajitafakari kwani chama
hicho kinahitaji watu wa maeneo hayo kurejeshewa imani na amani. Maeneo
hayo yamekumbwa na mauaji mfululizo ya viongozi wa CCM. Katibu wa
Sekretarieti, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hayo
jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia suala hilo.
Alisema CCM imekuwa inafuatilia kinachoendelea katika maeneo hayo na
kujiridhisha kuwa kuna haja ya Serikali na vyombo vya ulinzi kuongeza
umahiri, ubunifu na weledi wa kushughulia uhalifu huo ili usiendelee.
“Tunatoa rai kubwa kwa serikali, tumevumilia, tumekaa kimya na
kufuatilia sana suala hili, Watanzania wanakufa, tunataka kuona kitu
kinatokea chenye kurudisha amani na hata imani kwa wananchi,” alisema
Polepole.
Alisema wananchi wa maeneo hayo wanaishi kwa hofu huku wengine
wakikimbia nyumba zao ilhali ni haohao waliomchagua Rais John Magufuli,
hivyo wana haki ya kuwa na maisha yenye amani kila siku. Alisema kama
suala hilo ni ujambazi au ujangili inatosha na ifikie mwisho kwani hiyo
ni moja ya namna nyingine kuhujumu wananchi na mali zao. Alisema vyombo
vya ulinzi na usalama vishirikiane kurejesha amani, ili uchaguzi wa CCM
unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ufanyike salama.
“Kazi ya chama madhubuti ni kuwasemea watu, wapo waliouawa kikatili
na watu wasio na mioyo, hisia wala utu wakati hakuna dini inayoamini
katika kutoa uhai wa mtu isipokuwa Mungu pekee,” alisema Polepole.
Alituma salamu za pole kwa wote walioathirika na uhalifu huo wakiwemo
viongozi na wanachama wa chama hicho ambao wamepoteza uhai.
No comments:
Post a Comment