Apatikana akisafirisha mikono ya binadamu China
Maafisa wa usalama kusini magharibi mwa China walipigwa na butwaa hivi majuzi walipogundua mwanaume mmoja alikuwa akisafirisha mikono miwili ya binadamu.
Kwa mujibu wa Pear Video, mzee wa miaka 50 kwa jina Zheng alisimamishwa na maafisa wa polisi katika kituo cha mabasi cha Duyun, katika mkoa wa Guizhou baada ya mikono miwili ya binadamu kugunduliwa na mtambo wa kiusalama tarehe 31 Julai."Nilimuuliza alikuwa amebeba nini kwenye mkoba wake, na akanijibu kwamba ulikuwa ni mkono," afisa wa usalama aliambia Pear Video.
Kwa mujibu wa gazeti la South China Morning Post, alizuiliwa mara moja, wakimshuku kuwa huenda alikuwa amehusika katika mauaji.
Bw Zheng alisema kakake aliomba asaidiwe kusafirisha mikono hiyo hadi alikokuwa akiishi, ili atakapofariki, mwili wake na viungo hivyo, vizikwe eneo moja.
Bw Zheng aliachiliwa huru na maafisa wa serikali baada ya hospitali iliyokuwa ikimtibu kakaake kuthibitisha kisa hicho.
Nchini China, watu huamini kwamba mwili unafaa kuchomwa ukiwa mzima au kuzikwa pia ukiwa mzima ndipo marehemu awe na amani.
Hata hivyo, wengi wa waliosoma taarifa hiyo mtandaoni wameshangazwa sana na kisa hicho, ikizingatiwa kwamba maafisa wa matibabu huhitaji kibali maalum kuruhusiwa kusafirisha viungo vya binadamu.
No comments:
Post a Comment