Header Ads

Majaliwa aagiza sensa ya mifugo

MuroTv

Majaliwa aagiza sensa ya mifugo

04 Juni 2017
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza maofisa mifugo kufanya sensa ya mifugo nchini na kubaini idadi yake ili sekta hiyo iweze kuendeshwa kwa tija na kuepusha migogoro.
Alitoa kauli hiyo katika maeneo tofauti wilayani Gairo mkoani Morogoro katika ziara yake kukagua miradi ya maendeleo. Alisema pamoja na kufanya sensa hiyo, maofisa hao wakae na wenye mifugo, kuwashawishi kuwa na mifugo inayoendana na eneo walilonalo kwa ajili ya malisho.
Kwamba sensa hiyo itasaidia mpango mkakati wa serikali wa kuinua sekta ya mifugo kwa kuipatia mahitaji yake muhimu kama tiba, malambo na majosho kwa kulingana na idadi. Alipongeza kampeni ya utambuzi wa mifugo iliyofanywa na mkoa wa Morogoro, iliyofanyika hivi karibuni.
Kwamba kazi hiyo imewezesha kupata takwimu na mwenendo wa mifugo kwa lengo la kutengeneza mkakati wa kuondoa kero za malisho na migongano ya wakulima na wafugaji. Mkoa wa Morogoro unajulikana kwa kuwa na maeneo yenye migongano katika ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Wakati huohuo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari ameagizwa aitishe kikao na uongozi wa Halmashauri ya Kilosa na kupata kauli yao ni lini watalipa zaidi ya Sh milioni 210 wanazodaiwa na Halmashauri ya Gairo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Morogoro, wilaya ya Gairo na watumishi wa Halmashauri ya Gairo baada ya kupokea taarifa ya mkoa na wilaya katika kikao kilichofanyika Gairo mjini.
“Kilosa ni lazima wazilipe hizo fedha. Katibu Tawala simamia zoezi hilo na kama watachelewa, uzikate moja kwa moja kwenye fedha yao wanayoletewa kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI).
Nataka nipewe taarifa ya maamuzi hayo kabla Juni haijaisha,” amesema. Mapema akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe alisema wanaidai Halmashauri ya Kilosa sh 233,228,679 ambazo ziliingizwa huko wakati wilaya hiyo inaanzishwa na hawakuwa wamefungua akaunti ya wilaya.

No comments:

Powered by Blogger.