Header Ads

WAZIRI MBARAWA AZINDUA BIDI DMI

Waziri Mbarawa azindua Bodi DMI

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
 
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amezindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na kuwataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na uwazi ili kuiendeleza nchi.
Akizindua Bodi hiyo jana jijini Dar es Salaam, Profesa Mbarawa alisema wajumbe wapya wa Bodi hiyo wana nafasi ya kukipeleka chuo mbele zaidi huku akiwashukuru wajumbe waliomaliza muda wao kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Bodi hiyo inaundwa na wajumbe watano. “Natoa ushauri huu si kama Waziri tu, bali pia kama mdau wa sekta hii, kwani nimejihushisha na shughuli za usafiri wa meli kwa muda mrefu sasa, ninaifahamu vema sekta hii,” alisema.
Wajumbe walioteuliwa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Ernest Bupamba ni Dk Mwamini Tulli, Tumaini Silaa, Alfred Misana na Andre Matillya. Alisema pamoja na changamoto mbalimbali ambazo chuo inakabiliana nazo kama vile uhaba wa miundombinu ya kufundishia ikiwamo uhaba wa majengo na ufinyu wa bajeti ya mafunzo, atashirikiana na Bodi ya chuo hicho katika kukabiliana na changamoto hizo.
“Nitashirikiana na bodi yenu, chini ya nahodha mzoefu Bupamba na ni matumaini yangu kwamba kwa pamoja tutaweza kukabiliana nazo,” alisema waziri. Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bupamba alimhakikishia Profesa Mbawara kuwa taasisi yake itashirikiana na Serikali kuhakikisha malengo ya chuo hicho yanafikiwa.
Mkuu wa Chuo hicho, Dk Erick Massami alisema taasisi yake imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kwamba inatoa kozi mbalimbali kwa viwango vya cheti hadi shahada.

No comments:

Powered by Blogger.