Na Salym Juma, Arusha
Tar 6 July 2017 ilikuwa siku nzuri kwa ‘Mashetani’ kwani walifanikiwa kunasa saini ya bidhaa adimu kwa sasa ulimwenguni. Kumpata mtu aliyefunga magoli 26 katika michezo 39 kwa sasa sio jambo jepesi. Kumpata mshambuliaji mwenye nidhamu nzuri, mwenye nguvu na kipaji cha umaliziaji sio jambo rahisi kama unavyofikiri. £75 million zinaweza kuwa sahihi japo bado msimu haujaanza. Lukaku alitajwa sana kwenda darajani ila mwisho wa siku anatua ‘OT’. Watu wengi wameshangazwa na hili na wengine wanatamani habari hii iwe tetesi ila haiwezi tena kwani tayari Lukaku ameshakabidhiwa jezi ya ‘OT’.
Kutokana na ughafla huu, mashabiki wa Chelsea hampaswi kumlaumu Lukaku kwani huenda kuna vingi chini ya kapeti na leo hii nimejaribu kutazama sababu ambazo zimechangia kukamilika kwa dili hili ambalo ni rekodi kwa Everton.
Dili la Whyne Rooney kurudi Everton limechagiza kukamilisha uhamisho wa Lukaku kwani Everton wanaamini Rooney atawasaidia sana nje ya uwanja kuliko hata ndani kutokana na uwezo wake kuwa ukingoni. Endapo Lukaku angeenda Chelsea au timu nyingine sina hata tone ya shaka kwamba Mourinho angeridhia kwa roho moja Rooney kwenda Everton. Uhitaji wa Everton kwa mshambuliaji Rooney ni mkubwa kwani ndoto ya Everton ni kutaka kuona kijana wao waliomkuza anarejea nyumbani na kumalizia karia yake pale na sio kwenda klabu nyingine hasa za pale England.
Everton wamekuwa wakiwageuka Chelsea dakika za mwisho siku za karibuni katika biashara ya kuuziana wachezaji. Nani asiejua dili la John Stone kwenda Chelsea? ‘The blues’ walifika dau kila Everton walipopandisha tena zaidi ya mara tatu ila mwisho wa siku Dunia ilishangaa kijana huyu kwenda Etihad kwa £47.5m pesa ambayo ilikuwa kawaida sana kwa Chelsea. Kumbuka Everton waliwahi kukataa £60m za Chelsea kwa beki huyu ambaye amekuwa na msimu usioridhisha pale Manchester kutokana na makosa kadhaa ambayo huenda yanachagizwa na ‘Pacha’ anayecheza naye pale kati.
Kuna taarifa za ndani ambazo nalazimika kuziamini baada ya dili hili kukamilika kwamba Lukaku alikuwa anatakiwa zaidi na Michael Emenalo pamoja na baadhi ya viongozi wa Chelsea ila hakuwa chaguo la kwanza kwa muitaliano Conte. Michael Emenalo ni Mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea na siku za karibuni amekuwa akishutumiwa na wapenzi wa Chelsea kwa kuchelewesha usajili. Emenalo amekuwa akipishana na Conte tangu dirisha dogo. Morata ndiye alikuwa chaguo namba moja la Conte kutokana na uzoefu aliokuwa nao Alvaro kwenye michuano ya Ulaya na pia aliwahi kufanya kazi na Conte.
Lukaku hakupata matumaini ya kurudi Chelsea hasa kutokana na Conte kutoonesha ushirikiano wa karibu na mchezaji huyu hasa baada ya msimu kukamilika. Kuna wakati Lukaku ‘aliwa-follow’ wachezaji wa Chelsea kwenye mtandao wa Twitter ila Morata naye kuna kipindi alifanya hivo pia na huenda hii ilimuaminisha Lukaku kwamba huenda yeye sio chaguo namba moja kwa Conte. udhaifu huu ndio umetumiwa vyema na Mourinho kunasa saini ya Lukaku hasa akiamini atakusanya pointi nyingi kwenye ‘timu ndogo’ za Premier kama ilivyo kawaida ya Lukaku.
Lukaku anadai ana mahusiano mazuri na Mourinho kwani usajili wake wa kwenda Everton masaa machache baada ya kukosa penalt kwenye mechi ya Uefa Super Cup dhidi ya Bayern Munich ya Guardiola uliamuliwa na yeye na sio Mou. Chelsea ilimlaumu Mou baada ya Lukaku ‘ku-shine’ Everton ila Lukaku anadai amerudi kwa Mou kutokana na uhusiano mwema walionao tangu Chelsea ndio maana imekuwa rahisi usajili huu kukamilika. Mourinho japo hakumsajili Lukaku Chelsea ila alimrudisha mwaka 2013 kutoka West Bromwich Albion jambo ambalo linampa moyo Lukaku kufanya kazi na Mou.
Michael Keane, Morgan Schneiderlin, Rooney na Fellain ni baadhi ya Wachezaji wa karibuni ambao vilabu hivi vimeuziana. Hii ina maana pana sana kwenye usajili wa Lukaku kwani mbali  na sababu binafsi za Lukaku kwenda United, Raiola, uongozi wa Everton umechangia pakubwa kukamilika kwa usajili huu ambao huenda ukawasaidia United msimu ujao. Wazungu huwa wanathamini mahusiano mazuri kibiashara linapokuja suala la ziada kama ilivyokuwa kwa Lukaku. Kumbuka Everton ni mahasimu wa Liverpool, Man United pia ni mahasimu wa Liver, umegundua nini hapo?
Yote kwa yote usajili wa Lukaku kwenda United haukuja kwa bahati nasibu kwani Mourinho alipendekeza jina la mbelgiji huyu mwenye asili ya DRC mapema sana kabla hata ya Morata na CR7. Majeraha ya Ibrahmovich yalimfanya Mou kukesha na watendaji wa Man United ili apate saini ya Lukaku hasa pale aliposikia Chelsea wanamuhitaji. Kumbuka Mou alikomaa na saini ya Pogba baada ya kusikia Chelsea wanamuhitaji. Mou pia alijaribu kumshawishi Kante asiende Chelsea. Huenda lengo la Mou kuibomoa Chelsea nje ya uwanja likakamilika kwani bado anamtaka Morata (Teh teh teh)