Header Ads

KINACHOJULIKANA LEO NI KIKUBWA UKILINGANISHA NA KILICHOJULIKANA JANA

Kinachojulikana leo ni kikubwa ukilinganisha na kilichojulikana jana

TUNAISHI katika kizazi ambacho fikra zake zimetekwa na uwezo mkubwa wa sayansi. Ni kweli kwamba watu wa mabara mengine tofauti na Afrika ndiyo hasa waliotekwa na mawazo hayo kuwa sayansi ni jibu la kila kitu. Hii ni kwa sababu idadi kubwa miongoni mwetu siyo wasomi kama walivyo watu wa Amerika, Ulaya, Australia au nyingi ya nchi za Asia. Lakini fikra hizi za kutukuza sana sayansi zinaanza kuchomoza hata huku nyumbani kwa vile dunia imekuwa kijiji.

Fikra hizi ni hasa juu ya mawazo kuwa, matatizo yote ya mwanadamu yanaweza kutatuliwa kwa nyenzo za kisayansi. Tayari sayansi imeonyesha mafanikio makubwa sana katika nyanja nyingi. Kwa wanaotazama historia ya miaka au karne zilizopita, wanaona uvumbuzi mpya unavyotupatia urahisi wa maisha kulinganisha na huko tulikotoka.

Fikiria tu kuhusu teknolojia ya mawasiliano ilivyorahisishwa. Alafu tazama tena uwanja wa afya. Maendeleo makubwa kudhibiti magonjwa au kuyaponya. Hata huko Ulaya historia yao inawakumbusha namna magonjwa kama tauni yalivyowahi kuwanyanyasa. Huduma za afya zimekuwa njema na kuna baadhi ya magonjwa ambayo yanabakia kuwa historia katika baadhi ya jamii.

Mafanikio haya dhahiri ya sayansi yapo pia katika namna binadamu anavyouelewa ulimwengu. Kwa sasa mengi yanaeleweka kuhusu anga za juu, na ingawa bila shaka yapo mengine mengi zaidi yasiyoeleweka, lakini safari ya kuyaelewa inaendelea. Hata kama haidhaniwi kwamba itatokea siku sayansi ikayaelewa yote, kinachojulikana leo ni kikubwa sana ukilinganisha na kilichojulikana jana.
Kuelewa ukweli kuhusu anga za juu ni muhimu sana kwa sababu imani nyingi za ustaarabu wa kale ulihusisha anga za juu na nguvu za miungu. Kilichotazamwa kwa hofu, kwamba kudra zinatoka huko (angani) sasa kinatazamwa kisayansi.

Mafanikio haya yanafurahisha kwa kweli. Unyonge wetu mbele ya ulimwengu umepungua sana. Lakini, hata hivyo, haya ni mafanikio ambayo lazima yachukuliwe kwa tahadhari. Dr S. Jayard, mwalimu wa falsafa ya sayansi, anaonya kuwa yapo maswali magumu ambayo sayansi haina uwezo wa kuyasogelea, sembuse kuyatafutia suluhu. Hapa tunaweza kufikiria kuhusu swali maarufu, muhimu mno, na la kale sana la kifalsafa; lengo la maisha ni nini?

Karne baada ya karne, na vizazi tofauti vimekuwa vikijaribu kujibu swali hili, kwa namna tofauti tofauti. Tamaduni nyingi zikiegemea imani kama msaada wa kujua maana ya maisha, na wengine wakiunda mirengo tofautitofauti ya kifalsafa kusudi kuelezea maana hasa ya maisha. Hata katika karne hii ambayo sayansi imekomaa sana, bado haiwezi kutuambia lengo la maisha ni nini.
Ikiwa sayansi inakwama katika maswali magumu yanayohusu maisha, bado tena inakwama vibaya zaidi katika matatizo makubwa sana yanayosababishwa na sayansi yenyewe. Hapa, kwa mujibu wa Dr. Jayard, sayansi haiwezi kuyashughulikia kwa vile ni sayansi yenyewe iliyoyaunda.

Ubovu uliozalishwa na sayansi, unahitaji nguvu ya nje kuurekebisha. Tatizo kubwa sana linasobabishwa na sayansi ni kwa sababu ya kile kiitwacho “scientism” au kwa tafsiri yangu, ‘udikteta wa sayansi’. Hapa, sayansi hupenda kujinyakulia mamlaka ya kuelezea kila kitu na kukataa kila kitu kisichoweza kuingia katika vipimo vya kisayansi, vya kimantiki na vya kimahesabu.

Udikteta huu wa sayansi huingia katika nyanja nyingi sana za kitaaluma. Tena taaluma nyingi (kama siyo zote) hupenda kujinasibisha na sayansi. Ndipo tunapozishindilia taaluma zote katika makundi kama ya sayansi jamii (social sciences) na sayansi ya asili (natural science) ilimradi kuonyesha kwamba taaluma husika ni halali kwa vile tu inaenea katika vigezo vya kisayansi.

Hata elimu za maadili zimebanwa katika vipimo vya kisayansi. Ni hivi: kiutamaduni maadili ni suala pana sana ambalo lilisambaa katika katika kujibu binadamu ni nani, wajibu wake ni nini, na anakwenda wapi.

Afanyacho binadamu kilipaswa kupata angalizo la maswali hayo yaliyotangulia. Ndipo falsafa ya magharibi, (nadhani hata ya mashariki) zilipozungumza kuhusu maadili kwa kuegemea sheria ya maumbile (natural law) sheria ya Mungu (divine law) na sheria za kibinadamu kulingana na mahitaji (positive law). Baada ya udikteta wa sayansi, kizazi chetu kinataka kubakiza ‘positive law’ pekee.

Sheria ya Mungu na sheria ya maumbile inapigwa teke. Kama tunadhani magharibi pekee ndiyo wanaofanya hivyo, tujue kuwa hata hapa kwetu mawazo haya ya kukumbatia ‘positive law’ yapo. Kwa maoni yangu, maadili hayo yanayoegemea katika sheria ya Mungu ya maumbile, yanakataliwa kwa sababu ya udikteta wa sayansi.

Mungu hawezi kuthibitishwa kisayansi. Kadhalika hata hivyo viitwavyo sheria ya maumbile, havipo sawa kwa watu wote – kwa mujibu wa udikteta wa sayansi. (ninapotumia maneno ‘positive law’, natural law na divine law, narejea hasa muktadha wa wanafalsafa wa magharibi wa karne za kati)

Nitaelezea jambo hili gumu, athari ya udikteta wa sayansi, kwa simulizi rahisi ya ukweli. Mwalimu mmoja toka ng’ambo alikuwa anajitolea kufundisha hapa Tanzania, miaka zaidi ya kumi iliyopita. Alitembelewa na binti yake aliyetaka kuona mazingira na wanafunzi ambao baba yake anawafundisha.

Katika kubadilishana mawazo na wanafunzi, binti aliulizwa swali: ‘unategemea kupata watoto wangapi pindi utakapoolewa?’ binti alijibu: ‘sitegemei kuwa na mtoto, labda itokee kuwa kutakuwepo uwezekano wa kubadilishana mimba kwa zamu mimi na mume wangu. Lakini vinginevyo naona hamna usawa mimi peke yangu kuwajibika kubeba mimba kwa miezi tisa’.
Baba yake alisikitika kwa majibu ya binti huyu. Na akadokeza kuwa, katika nchi yake, hili siyo tatizo la binti huyu pekee bali ni mawazo yanayojijenga miongoni mwa vijana wengi wa rika lake. Binafsi nimehusisha msimamo huu unaohuzunisha wa binti huyu na kile kilichotangazwa huko Spain majuzi – kuna wizara iliundwa kushughulikia watoto wazaliwe. Nchi ina upungufu wa watoto.

Tunasema hili ni tatizo kubwa na kwa kiasi kikubwa limesababishwa na namna ya kufikiri kisayansi, katika hali ambayo sayansi haiwezi kusaidia kutoa suluhisho la kimaadili, S. Jeyard, katika jambo kama hili angesema kuwa, suluhisho ni “moyo wa kibinadamu na wala siyo maabara ya kuhamisha mimba, kwamba zamu moja ikae kwa baba, zamu nyingine ikae kwa mama”. Huenda mfano huu unaweza uonekane kuwa hautuhusu sana hapa nyumbani, lakini kwa kweli mawazo ya aina hiyo yalishaanza kupiga hodi.

Kwa kufuatilia mijadala kadhaa, na kuwasikiliza vijana kadhaa, na maswali wanayouliza, na majibu wanayoyataka, hasa eneo la maadili, unaona kuwa udikteta wa sayansi unaingia hata huku kwetu – iwe kwa kujua au kwa kutokujua.

Tunaingiwa na kishawishi cha kutaka kuweka fumbo la ukweli wa maisha katika ‘precision’ yaani lielezeka kana kwamba tunaelezea ukweli wa kimahesabu. Fumbo la maisha wakati mwingine halifuati mantiki, wala halielezeki kimahesabu.  Sayansi haitoshi kuuweka ukweli wote ndani yake kama vile barua inavyowekwa ndani ya bahasha.

Nihitimishe kwa Hadithi moja ya mwandishi wa Mumbai India: siku moja tembo alikuwa anafurahia ubaridi wa maji katika bwawa huko porini. Akaja panya, akikaa kando ya bwawa, akamsihi tembo atoke nje ya maji. Tembo akasema “sitoki”.

Panya akaendelea kusisitiza – “tafadhali toka, kuna jambo la muhimu nataka kukueleza, ila ni lazima uwe nje ya bwawa” tembo akaonyesha msimamo kwamba hawezi kutoka, na zaidi ya hayo, hilo jambo la muhimu anaweza kulisikia hata akiwa ndani ya dimbwi.

Baada ya panya kusisitiza sana, tembo akaona isiwe shida, akatoka nje ya maji na kutaka kusikia hiyo habari ya panya. Panya akasema; “nilitaka tu kujua kama umevaa kaptura yangu ya kuogelea”. Anthony de Mello SJ, mwandishi wa simulizi hili anamalizia kwa fundisho: “ni rahisi zaidi kwa kaptura ya panya kumtosha tembo kuliko kuliko maarifa yetu kuweza kuelezea kuhusu Muumba/Mungu bila kumbakiza.”

Kwa maneno mengine, akili yetu haiwezi kuelezea mafumbo yote kwa ukamilifu,  bali itajaribu tu kugusa sehemu. Badala ya kumtaja ‘Mungu’ kuelezeka na akili ya kibinadamu kama De Mello alivyomtaja kwenye hadithi yake hii, tunaweza kusema ‘fumbo la maisha’ halielezeki lote kisayansi.
Sayansi inaelezea sehemu tu. Na hivyo inaweza kusaidia kutunga sehemu tu ya sheria. Bado tunahitaji sheria kutoka nje ya utawala wa sayansi, ingawa sayansi yaweza kusaidia kuziboresha.




No comments:

Powered by Blogger.