5 WAFARIKI KWA KUGONGWA NA GARI, KUCHOMWA VISU
Muro Tv
5 wafariki kwa kugongwa na gari, kuchomwa visu
WATU watano wakazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara wamefariki dunia
katika matukio matatu tofauti juzi na jana watatu wakigongwa na gari na
wengine kuchomwa visu sehemu mbalimbali.
Waliogongwa na gari ni Bhoke Burure (22) mkazi wa Kijiji cha Magena
na Chacha Marwa mwendesha bodaboda yenye namba za usajili MC722 AYU aina
ya Sun LG wa Kijiji cha Itebe Magena. Mwingine ni mwendesha baiskeli
ambaye jina halikufahamika. Waligongwa na gari aina ya Probox yenye
namba T358 DHV iliyokuwa ikiendeshwa na John Mangera.
Pia wanawake Bhoke Chacha (30) mkazi wa Kijiji cha Magoma na Ghati
Mwita (24) wa Kijiji cha Mogabiri waliuawa kwa kuchinjwa na mwingine kwa
kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili. Umati mkubwa wa wananchi
ulifika kuona na kutambua miili ya marehemu hao katika hospitali ya
wilaya Tarime. Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Mkumbo Luther
alikiri kupokea miili hiyo.
“Tumepokea miili ya watu watano jana (juzi). Ipo hapa chumba cha
maiti, minne kati yake imetambuliwa na ndugu zake. Marehemu
waliotambuliwa ni wa ajali ya gari iliyotokea mchana katika Kijiji cha
Magena Kata ya Nkende. Waliotambuliwa ni Bhoke Burure mkazi wa Kijiji
cha Magena aliyekuwa mjamzito, na mwendesha bodaboda, Chacha Marwa mkazi
wa Kijiji cha Magena,” alisema.
Aliwataja marehemu wengine kuwa ni ya kijana wa miaka kati ya 20 - 25
ambaye hajatambuliwa jina lake na makazi yake, wanawake Bhoke Chacha
aliyekutwa ameuawa kwa kuchinjwa shingo na mwili wake kutupwa kando ya
barabara itokayo Nyamwigura na Mogabiri na Ghati Mwita aliyeuawa Kijiji
cha Nyangoto Nyamongo kwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Aliwataja majeruhi wawili waliolazwa kutokana na kujeruhiwa katika
tukio hilo kuwa ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Magena, Frank Mwita
(12) aliyeumia sehemu mbalimbali za mwili na mwanamke raia wa Kenya,
Carelin Adhiambo kutoka Rongo Mkoa wa Nyanza ambaye amejeruhiwa
mgongoni.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Sweetbert Njewike
alithibitisha kutokea kwa ajali hizo. Alisema dereva na mmiliki wa gari
la Probox lililosababisha ajali hiyo, John Mangera alitoroka na
anaendelea kutafutwa huku uchunguzi ukifanywa kuhusu mauaji ya wanawake
hao.

No comments:
Post a Comment