Wanafunzi wanaomba kujiunga na vyuo vikuu: Je, ukasome shahada na chuo gani?
Na Prosper Muro
Vyuo vikuu vya Tanzania vimefungua madirisha ya usajili mpya kwa ajili ya muhula wa masomo wa mwaka 2017/2018. Sio vyuo vya Tanzania tu bali karibu nchi nyingi huu ndio muhua wa kudahili wanafunzi wapya. Hiki ni kipindi muhum sana kwa vijana wetu hasa wanaoanza shahada ya kwanza kwani ile ndoto yao ya kupata “DEGREE” na kuwa “MSOMI” ndio inaanza kuwa na ukweli. Hivyo ni muhim sana vijana hawa wakapata mwangaza wa kutosha wanapochagua chuo gani cha kujiunga na kwa ajili ya kusoma programme gani.
Wale walio kwenye vyuo vikuu wanaelewa changamoto ambazo huwa tunakutana nazo kama waalimu/wahadhiri nyakati kama hizi. Wanafunzi wengi hawajui wakasome programme gani na kwa nini. Hili tatizo sio dogo kwani mara nyingine tunafundisha wanafunzi madarasani ambao hawajui walichochagua kusoma kinawapeleka wapi. Wengi hawajui nini iwe msingi wa maamuzi ya chuo gani cha kusoma. Mbaya zaidi, mara nyingi vijana hawa wanashauriana wao kwa wao au kushauriwa na watu wasio na uelewa wa mambo ya kitaalamu kwa taarifa zisizokua sahihi, zisizokua na ukweli, na za kupotoshana. Wako vijana wengi wamefeli chuo kikuu sio kwa sababu hawana uwezo bali kwa kuwa walijipachika kusoma vitu ambavyo havimo ndani yao bali walijiunga kwa mkombo, kutokujua au kushauriwa vibaya.
Yako maswali ambayo vijana wengi wanaotaka kuingia Chuo Kikuu hujiuliza. Na maswali haya huwa magumu hasa kwa wale ambao wana ufaulu mzuri unaowaruhusu kusoma chuo chochote au programme yoyote kwenye eneo lao. Nichague programme gani? Kwa nini? Itanipeleka wapi baada ya kupata degree? Je, nisome chuo gani kama inapatikana kwenye vyuo vingi? Ngoja nitaje mambo kadhaa ambayo yanavyoweza kumsaidia mtu kufanya maamuzi ya nini cha kusoma na akasome wapi.
- Kitu cha kwanza, kijana afahamu kwamba degree ya kwanza sio mwisho
wa reli (sio mwisho wa kuelemika) bali ni kuingia kwenye reli
(inakuingiza kwenye ulimwengu wa taaluma na kukufungua fahamu juu ya
machaguo yaliyo mbele yako). Kijana akilijua hili na kutumia vizuri muda
wake wa miaka 3 au 4 chuo kikuu, haitajalisha sana kasoma shahada gani
kwani atatoka na zaidi ya cheti chenye jina la shahada
- Pili, kijana ajue HAKUNA SHAHADA ISIYOKUA NA TIJA/KAZI/MAANA
katika uhalisia wa maisha na taaluma. Vijana wanaokuja kutafuta ushauri
wangu kuhusu kuchagua nini cha kusoma, huwa naaambia hata kama kuna
shahada ya kucheza maigizo tu au kuimba tu au kukimbia tu, bado inaweza
kubadilisha maisha yako kuliko aliyefanya medicine, au uhandisi au
kingine. Ila hili litaeleweka iwapo tu point ya kwanza imeeleweka.
- Tatu, ukishaelewa points mbili hapo juu, kijana atambue kwamba
HATUSOMI SHAHADA ILI TUAJIRIWE. Shahada sio mafunzo ya kuajiriwa bali ni
nafasi ya kupata elimu ya juu na uelewa mkubwa zaidi wa maisha na dunia
kama nyenzo za kutafuta maarifa zaidi ya kukusaidia wewe, familia yako,
jamii, taifa lako na mwisho wa siku kuifanya dunia yako na wengine kuwa
mahali pazuri pa kuishi. Ni kweli kwamba tunataka ajira baada ya kupata
shahada lakini ukisoma chuo kikuu kwa malengo ya maandalizi ya
kuajiriwa pekee unajiweka kwenye nafasi kubwa sana ya kuwa frustrated
baadaye.
- Nne, kitu cha msingi sana kumsaidia kijana kuchagua degree ya
kusoma, ni kile kitu anachokisikia ndani mwake kama wito wake wa maisha
(wengine wanaita VIPAWA). Hili swali hutakiwa kuchokozwa ndani ya vijana
tangu wakiwa wadogo na mashuleni na kusaidiwa kujenga msingi wa
kuelekea huko wanapoelekea elimu za juu. Niseme tu kwmaba hii ndio
tofautikubwa sana ya wasomi katika nchi zetu na wengine waliotutangulia
hasa Ulaya na Amerika. Ndio mana katika shule zao za msingi na
sekondari, vijana wanakuwa exposed kwenye mambo mengi sana na huko kila
mmoja anakutan ana kinachoendana na maono na vipawa vyake.
Ila nasema hili nikitambua kwmaba wengi wetu (pamoja na mimi) hawajapata hiyo nafasi ya kufundishwa au kulelewa kulingana na vipawa vyao na wengi wamejikuta wakisoma kwa kubahatisha zaidi. Kijana akisoma degree yenye contents zinazoendana na kile anachokisikia ndani mwake, ana nafasi kubwa sana ya kufanikiwa kimaisha kuliko ambaye kasoma degree kwa sababu tu ana akili/uwezo wa kusoma programme husika. Zaidi sana, mtu huyu anaishi maisha ya kuridhika sana na ana uwezo mkuwa wa kuwa mbunifu katika maisha.
- Tano, ni kosa kubwa sana kuchagua degree KWA KUTAZAMA JINA LA
DEGREE. Nina ujasiri wa kusema kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi wa
vyuo vyetu wanachagua cha kusoma kwa kutazama jina la programme na mara
nyingi hata hawajui inawapeleka wapi. Nimeshauri vijana wengi wanaojuta
kusoma degree walizosoma na kuona walipoteza muda wao. Nimesoma na watu
ambao hadi wanamaliza degree ndani mwao walikua wanajuta na hawajawahi
kupata amani na walichokua wanasoma. Nimeona wanafunzi wakiingia chuo
kikuu na kuanza kutapatapa kutafuta mpango wa kubadilisha degree
walizodahiliwa maana wanajiona haziendani nao au hazifanani na
walichokua wanadhani watapata. Wako wengine waliamua kabisa kuachana na
biashara ya degree wakarudi mtaani. Kama nilivyosema awali, degree
inakupa mwanga wa kitaalama na kukupa nafasi ya kutumia vema vipawa
vilivyo ndani yako. Hivyo chagua programme inayokwenda kulea kile
kilichoko ndani yako.
- Sita, usichaguliwe degree ya kusoma na mzazi, mlezi, ndugu, mhadhiri
au mtu mwingine yoyote ile. Hii ni ngazi ya muhum sana kwenye maisha
yako ambayo utaishi nayo hadi kifo. Acha watu wakushauri na jitahidi
kupata ushauri unaokusaidia wewe kufanya maamuzi mazuri na sio
kukulazimisha kuchukua maamuzi ya anayekushauri. Vijana wengi wanasoma
degree fulanifulani kwa kuwa wazazi wao wametaka au wanaona hizo ndio
degree zenye heshima zaidi au zitakazowapa kazi nzuri zaidi. Nina
ujasiri wa kukuambia kwamba huo ulimwengu umepitwa na wakati. Hakuna
degree yenye heshima kuliko nyingine. HESHIMA YA DEGREE ANAIBEBA MTU NA
SIO JINA LA DEGREE AU UTALAAMU ANAOUPATA AU CHUO ALICHOKISOMA.
Nilipokua sekondari enzi hizo, tulisimuliwa habari ya kijana aliyelazimishwa na baba yake akasome sheria kwa kuwa aliona ndio degree yenye heshima/maana zaidi lakini haikua moyoni mwa kijanaa. Kijana alikwenda kusoma na alipomaliza alimpelekea baba yake cheti cha degree ya sheria halafu akamwambia ailikua anasoma kwa ajili yake lakini sasa ngoja arudi chuoni akasome kwa ajili yake. Nilipokua nasoma shahada ya kwanza nilishangaa kusoma na mtu ambaye alipomaliza kidato cha sita aliniacha nikiwa kidato cha kwanza au cha pili. Nilipoulizia niliambiwa alisoma shahada fulani (iliyotokana na kufaulu kwake PCB) na alipomaliza alimua kurudi UDSM kusoma alichoona anakitaka. Ni hatari sana kupotea miaka 3/4/5/6 ukisoma kitu ambacho huna passion nacho na huna mpango wa kukifanyia kazi. Fanya mamuzi sahihi wakat huu ili usipoteze muda baadaye.
- Saba, usishawishiwe na wenzako (peers) juu ya uzuri wa shahada ya
kusoma. Hao bado hawana mwanga wa maisha kama ilivyo kwako. Tafauta watu
sahihi wa kukushauri ambao wamevuka hatua unayoiendea wewe. Nina ushuda
wa wanafunzi walisoma zilizoitwa shule maalum za enzi zile ambao
walikua wanakwenda kusoma degree kwa makundi (mobs) kwa kuwa tu walikua
wana ufaulu mzuri lakini wengi wao maisha yamekwenda kuwaonesha kwamba
walichemsha na sasa wamejielekeza mbali sana na walichosomea.
- Nane, kwamba uende chuo gani kusoma hili linaweza lisiwe na jibu
jepesi. Ila yako mambo kadhaa yanaweza kukusaidia. Moja, ni points ya 1
hadi 7 hapo juu. Hizi zaweza kukupa mwanga ya kujua ukasome wapi. Pili,
ni muhim sana kusoma chuo chenye miundombinu ya lazima kwa kile
unachokisomea. Vitu kama maktaba za kutosha, maabara, computer labs,
reliable internet connection, na vingine ni nyenzo muhim kukufikisha
kwenye ndoto yako. Hii ni changamoto maana vyuo vyetu vingi bado
vinajikongoja kimiundombinu ila kati ya hivyo unaweza kufanya maamuzi.
Tatu,soma chuo chenye wahadhiri wa kutosha kwenye field yako. Ni hatari
sana kusoma degree ukiwa unafundishwa na watu wenye degree moja au mbili
pekee. Hii ni taaluma (academics) na ni tofauti sana na kusomea
utaalamu mahususi (kama vile ufundi). Umefundishwa na wahadhiri wa aina
gani katika degree ya kwanza ni msingi mkubwa sana wa aina ya usomi
unaokwenda kua nao hasa usipopata nafasi ya kuendelea mbele zaidi.
Nasema hivi nikielewa tatizo kubwa la vyuo vingi kukosa wataalamu lakini viko ambavyo vinatoa programme huku wakiwa hawana kabisa wataalamu kwenye field hiyo. Hivyo ni vema ukafanya kautafiti kidogo kujiridhisha. Nne, unaweza ukawa na mahitaji maalum ya kiafya, umaskini na mengine ambayo ukisoma chuo fulani inaweza kukupa urahisi kuliko kingine. Tano, nisijifanye sijui. Ukweli ni kwamba viko vyuo ukisoma utapata shida sana kumwelewesha mtu kwamba hicho ni chuo kikuu au ni sekondari na shahada yake inaweza siwe na heshima kabisa mataani. Wako waajiri ambao wanalenga kuajiri wahitimu wa vyuo fulani tu kutokana na heshima ya kitaalamu vilivyojijengea. Ukiweza na kama una vigezo tamani kusoma huko. Sita, soma point ya tisa.
- Tisa, Kama unadhani unataka zaidi skills maalumu za kazi, basi
chagua vyuo vilivyojikita kwenye skills kuliko academics na sio lazima
usome degree. Vyuo vingi ambavyo zamani kabla hawajavigeuza kuwa vyuo
vikuu vilivyokua vinatoa certificates, FTC, diploma na advanced diploma
(mfano IFM, DIT, Mbeya Tech, TIA, IAA, Mzumbe, CBE, nk) ni vizuri kwenye
programmes zenye kukupa skills zaidi kwani ndio ulikua msingi wa
uanzishwaji wake (ingawa kwa sasa sio kwa kila programme maana navyo
vimevamia madegree). Ila kama unataka kubobea kwenye ulimwengu wa
academia, ku-philosophise, kujenga uwezo mkubwa wa tafakuri tunduizi
(critical thinking), ku-theorise, na mengine, basi nenda kwenye vyuo
vikuu kama UDSM, UDOM, SUA, na vingine vya ngazi hiyo maana vimejaa
wanazuoni waliobobea kukujenga kwenye upande huo. Ila pia kuna
programmes ambazo hazina mbadala wa vyuo. Kwa mfano kama unataka kuwa
daktari lazima uende miongoni mwa vyuo vichache tulivyonavyo vinavyotoa
programme hizo na zingine zihusianazo na tiba.
- Kumi, kuwa na matarajio sahihi kuhusu unachochagua kusoma. Mwaka
2009 nilikwenda kukagua wanafunzi walikua wanafanya mazoezi ya vitendo.
Kwenye moja ya taasisi nilizotembelea, nilikuta wanafunzi kadhaa wa
programme yangu (Computer Science and engineering) wakiwa na wanafunzi
wa vyuo vingine ambao wanasoma programme za TEHAMA (ICT). Miongoni mwao
wako waliokua wanasoma vyeti, stashahada na shahada kwenye vyuo ambavyo
vimejikita kwenye ufundi/ skills zaidi. Wale wanafunzi wangu wakaanza
kulalamika kwamba wao hawajui ufundi kama wenzako na hivyo wanaonekana
hawajui kitu.Na wenzao wakawa wanawaona UDSM sio kitu. Pia, nimewahi
kuona wanafunzi wa programme hizi wakilalamika kwamba hawajui hiki na
kile kwenye kwenye ufundi wa computer na ICT kwa ujumla. Kama vile
haitoshi, nimeshuhudia baadhi ya waajiri wakilalamika kwamba graduate wa
programme za vyuo fulanifulani kama computer science, computer
engineering, nk, hawajui kitu wakija kazini. Kibaya zaidi wanawapima
kujua kwao kwa vigezo vya ufundi na sio taaluma, uwezo wa
kiakili/ubunifu na uelewa walionao.
Ni vema mwanafunzi anayekwenda kusoma shahada ya sayansi ya compyuta akaelewa kwamba programme yake INAMTENGENEZA KUWA MWANASAYANSI WA KOMPYUTA zaidi na SIO FUNDI WA COMPUTER. Mwanasayansi pamoja na mambo mengine hujikita ndani sana kwenye nadharia ya anachosomea kuliko kile kinachoonekana kama kwenye ufundi. Hujengewa uwezo mkubwa wa kuelewa mambo magumu ya kitaaluma na kitaalamu ili awe na uwezo wa kufanya maamuzi na kutatua changamoto hata ambazo hajawahi kukutana nazo. Zao lake ni mtu ambaye unaweza kumtaka kujifunza chochote kipya na kigumu na akafanya hivyo kwa mafanikio na kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kujifunza ufundi (technician) ambayo hakua nao. Huyu ni tofauti sana na aliyejikita katika ufundi mahususi ambaye ukimpiga chenga kidogo tu unampoteza. Simaanishi kwamba huyu msomi wa computer science hawezi kuwa fundi (technician) au kujifunza ufundi, ila msingi wa elimu anayoipata wanapotoka chuoni sio kazi ya ufundi. Ni kosa na kutokuelewa mambo kumwona mhadhiri wa milolongotija (mechanical engineering) ni mjinga eti kwa sababu hawezi kutengeza gari kama fundi wako wa mtaani ambaye hakumaliza hata darasa la saba. A TECHNICIAN LABOURS TO KNOW HOW TO MEND THINGS but A SCIENTIST LABOURS TO KNOW HOW THINGS ARE MADE AND HOW TO MAKE THEM BE WHAT THEY ARE.
Nimeweka COMPUTER SCIENCE/ICT kama mfano tu lakini dhana hii yaweza kuwa kwa programmes nyingine pia. Elewa programme unayotaka kusoma inamaanisha nini na inakupeleka wapi na usiitafsiri kw ajina pekee ili uwe na matarajio sahihi.
- Kama unaweza au familia yako ina uwezo wa kifedha tafuta kusoma nje ya nchi hasa kwenye nchi zenye record nzuri kitaaluma. Pia kuna ufadhili (scholarships) nyingi sana duniani za shahada za kwanza na zingine zimelekezwa kabisa kwa nchi kama zetu ila watu wengi hawazijui na wengi hatujajizoea kukomaa kutafuta scholarships. Ila nitoe taadhari kwamba usiende kusoma chochote kwa sababu tu ni ulaya ua nje ya nchi. Hakikisha hata huko unasoma kitu chenye tija kwako na mazingira unayokuja kufanya kazi/ kutumika.
No comments:
Post a Comment