Mbinu za Kupata Mtaji wa Biashara
Na Prosper Muro
Watu wengi wanatamani kumiliki biashara siku moja na huenda wana
mipango mizuri juu ya bishara zao. Mipango hii inaweza ikawa vichwani tu
au mingine katika maadishi lakini inapofika wakati wa utekelezaji wa
mipango hii ukosefu wa mtaji wa biashara hiyo ni kipingamizi kwa wengi.
Lakini kuna jinsi kadhaa ambazo zinaweza kusaidia upatikanaji wa mitaji kwajili ya biashara.
Aina za Mitaji
Kuna aina mbili ya mitaji kwaajili ya biashara au uwekezaji wa aina yoyote.
- Mtaji wa Mkopo
- Mtaji wa Mmiliki
Mtaji wa Mkopo unakuwezesha kukopa toka kwa taasisi
za fedha au mtu binafsi wakiwemo ndugu ,jamaa na marafiki na kuhitajika
kulipa katika kipindi maalumu ikiwa pamoja na riba au bila riba.
Aina hii ya mtaji inakuwezesha kufanya biashara lakini ni lazima uwe
makini katika utunzaji wa fedha zako na uzalishaji wake kwani mwishowe
utahitajika kurudisha fedha zote pamoja na riba pengine kila mwezi.
Mtaji wa Mmiliki ni mtaji toka kwa mtu au kampuni
ambayo inahitaji kuwa na umiliki wa sehemu ya bishara. Hawa wanataka
kupata faida kutokana na uwekezaji katika kampuni au biashara yako.
Kama uko tayari kutoa sehemu ya umiliki wa biashara yako basi mtaji wa aina hii utakusaidia kuanzisha au kuboresha bishara yako.
Changamoto za Kupata Mitaji:
Kupata mtaji wa biashara ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali kote
duniani. Japo fedha za mikopo zinapatikana katika mabenki lakini bishara
nyingi hazina miundo mizuri na mifumo ya fedha kuwezesha kupata mikopo.
Benki zimekuwa na masharti magumu sana kiasi kwamba bishara nyingi
haziangalii huko kama sehemu ya kupata mikopo.
Mikopo toka kwa ndugu na jamaa pia ina changamoto zake,si rahisi
ndugu au rafiki akakuamini au akaamini kuwa biashara yako
itafanikiwa,tunajua asilimia 90 za biashara zinazoanza zinakufa kila
mwaka. Hili linawapa wasiwasi sana wakopeshaji.
Mambo ya Kuangalia kabla ya Kupata Mtaji
Mtaji toka kwenye Mikopo:
Ili kupata mikopo kunahitajika dhamana kuwahakikishia wakopeshaji
wako kuwa kama hutafanikiwa basi ni kwa jinsi gani fedha zao zitarudi.
Na utakutana na msharti mengi magumu,dhamana inaweza kuwa kama ifuatavyo:
- Nyumba
- Kiwanja
- Shamba
- Gari
- Mali za nyumbani au ofisini(biashara yenyewe)
Ni lazima ujiulize mapema kama uko tayari kuweka mojawapo ya vitu hivi kuwa dhamana.
Kwa namna hii ni rahisi kupata mkopo na ni lazima urudishe deni vinginevyo utapoteza.
Huu ndio ujasiriamali wenyewe, uthubutu wa kufanya mambo ya hatari katika harakati za kufanikiwa katika biashara.
Mtaji toka kwa Wawekezaji:
Kama utaamua kuingiza wawekezaji wengine katika biashara yako basi
pia nilazima ufikirie mapema kuwa kutakuwa na taarifa ambazo watahitaji
kujua juu ya mwenendo wa biashara yako.
- Je unapata faida kwa sasa?
- Muelekeo ukoje,unapanda na bidhaa au huduma zinahitajika?
- Ni kwa namna ipi fedha zinzohitajika zitawekezwa ili kuboresha biashara na kuleta faida kwa haraka n.k
Waekezaji nao wanaangalia hatari ya kupoteza fedha zao na pia muda wa kurudisha fedha wanazowekeza na faida itakayozalishwa.
Kama biashara yako haiwezi kuonyesha haya kabla,ni ngumu kupata wawekezaji katika bishara yako.
Mpango Bishara na utunzaji mzuri wa mahesabu ya biashara yako
yatasaidia sana kutoa taarifa hizi na hivyo kukusaidia kupata wawekezaji
Taarifa za Fedha na Mpango wa Bishara ni Nyenzo Muhimu Kupata Mtaji wa Biashara
Kama ni niashara mpya ,kutahitajika kuwa na mpango wa biahsara,andiko
ambalo linaelezea jinsi ambavyo biashara yako itafanyika ,kiasi cha
fedha kinachohitajika, bidhaa na huduma utakazo toa ,masoko,na
wafanyakazi.
Andiko hili litasaidia kushwawishi wawekezaji na watoa mikopo.
Kama biashara yako iko tayari na unataka kuongezea mtaji, basi
utahitaji kuwa na taarifa za hali ya fedha ya bishara yako, pia unaweza
ukaandaa mpango wa biashara unaoelezea mwelekeo wa biashara katika miaka
kadhaa mbele.
Wafanyabishara wengi wa kati na wa chini hawafanyi haya, ndio maana
kunakuwa na ugumu kupata mitaji ya kuanzia au kukuza biashara.
Huenda ukahitaji msaada toka kwa wataalamu wa biashara na upate
usaidizi wa kitaalamu,andaa fedha kidogo kwajili ya huduma hizi. Kuna
makampuni mengi tu sasa hivi ambayo yanatoa huduma kwa wafanyabiashara
kwa gharama ndogo.
Mbinu 5 za Kupata Mtaji wa Biashara:
Aina hizi zote za kupata mitaji zinaingia katika makundi mawili yaliyotajwa hapo awali aidha ni mkopo au uwekezaji
i. Mkopo toka Benki au Tasisi za Mikopo
Benki zote hutoa mikopo kwaajili ya biashara ila taarifa za muhimu
zinahitajika kuhusu mwenendo wa biashara kama tayari imeshaanza au
Mpango wa biashara unaoelezea jinsi ambavyo biashara itaendeshwa na
jinsi ambavyo deni litalipwa.
Benki huhitaji vitu vya thamani kwajili ya dhamana ya fedha watakazokupa kama mtaji.
Iwapo fedha hazitarudishwa kama ambavyo iliwekwa katika masharti ya mkopo basi mali hiyo itauzwa ili kufidia deni.
Hili limekuwa ni changamoto kwa wengi kupata mikopo toka benki. Hasa
kwa biashara anbazo zinaanza na hazina uhakika wa kufanya vizuri na
uwezo wake wa kurudisha deni.
Aina hii ya mikopo inaweza ikawasaidia wale ambao bishara zao
zimeshasimama na wanafanya kwa faida. Pia kwa zile biashara ambazo
mzunguko wa fedha ni mkubwa na hawatahitaji muda mrefu wa kulipa deni.
Benki mpya mara nyingi huwa na msharti rahisi kuliko benki kongwe.
Aina nyingine ya mikopo ambayo inafanana na ile ya benki ni toka
katika taasisi za mikopo. Taasisi hizi zinatoa masharti nafuu kido
kuliko yale ya benki. Nchini Tanzania kuna tasisi maarufu kama
FINCA,Blue ,Branc na nyingine nyingi ambazo zinatoa mikopo ya biashara.
Mara nyingine utahitaji kuwa katika vikundi ili kupata mikopo kwa urahisi au kuwa na biashara iliyosajiliwa kisheria.
ii. Mkopo toka kwa Ndugu,Jamaa au Marafiki
Ndugu na Marafiki ni sehemu nyingine ambayo unaweza kufikiria unapohitaji mtaji wa biashara.
Ni watu wanaokupenda na kukuamini na wako tayari kukusaidia katika
harakati zako za kufanikiwa kibiashara. Wako tayari kukusaidia kama wana
uwezo wakufanya hivyo. Lakini bado wanahitaji uhakika kuwa fedha zao
zitarudi. Watapenda kujua mpango wako na ni lazima uwe tayari
kuwajulisha,sio tu kabla hata baada ya kupata mkopo ili wajue mwenendo
wa fedha zao.
Kumbuka dhamana hapa haitakuwa mali bali uaminifu wako kwao.
Ukishindwa kufanya ulichoahidi utavunja uhusiano wenu mzuri uliojengeka
kwa muda mrefu.
Ni vyema kufikiria kwa makini kama utahitaji kuchagua njia hii,vinginevyo si njia nzuri sana.
iii. Toka katika Vikundi vya Kuweka na kukopa
Vyama vya Kuweka na Kukopa vinatoa mikopo kwa wanacama wake. Katika
vyama hivi wanachama wanatakiwa kuweka fedha katika akaunti zao.
Mwanachama anaruhusiwa kukopa kulingana na kiasi alichoweka. Baadhi ya
vyama vinaruhusu mwanachama kuchukua mkopo kufikia mara nne ya kiasi
alichoweka. Mkopo huu huwa na riba ndogo ulilinganishwa na benki.
Pia masharti yake si magumu na ya hatari kama ya benki.
Kuna vikundi vingine vya kijamii ambavyo wanachama wamekuwa wakifanya
hivyo na vinatoa fursa kwa wanachama kupata mitaji kwa kukopa.
Vikundi vya Kuchangiana:
Pia kuna mtindo wa kuchangiana kila mwezi ambapo wanachama katika
kikundi watachanga kiasi fulani cha fedha na kumpa mmoja wao ili afanya
kitu fulani muhimu ambacho asingeweza kwa kuwekeza binafsi.
iv. Mtaji toka kwa Wawekezaji Binafsi wa Nje
Kuna watu binafsi na makapuni ambayo tayari yanafedha na yanahitaji
kuwekeza katika biashara yenye kupata faida ili fedha zao ziongezeke.
Watu hawa wanaweka fedha benki ambako hazizai kwa riba nzuri
kulinganisha na biashara.
Watu hawa wanahitaji taarifa za kutosha kuwashawishi kuwa fedha zao
ziko katika mikono sahihi. Pia hata baada ya kuwekeza watahitaji taarifa
za mara kwa mara juu ya maendeleo ya biashara. Kama biashara ni mbaya
huenda wakatoa fedha zao ili wasipate hasara.
Hii ni sehemu nyingine ambayo huwa haiangaliwi sana na wajasiriamali
wadogo kwani ile dhana ya kufanya biashara kwa kushirikiana bado
haijakubalika na kufuatwa. Lakini njia hii inatoa nafasi kwa wale ambao
wanabiashara yenye mfumo mzuri na inakosa mtaji tu kufanikiwa.
Lakini hata kwa biashara zinazoanza, kama kuna mpango mzuri na wazo
lenyewe la bishara linaonyesha kufanikiwa basi wawekezaji hawa watakuwa
tayari kuwekeza katika biashara yako.
Hii ni njia nzuri kwa wale wenye uwezo wa kubuni biashara nzuri zenye
kutoa huduma kwa watu na yenye nafasi kubwa ya mafanikio lakini
wanakosa fedha za kuanzia. Hawa wanaweza wakaanza hata bila kuwa na
shilingi moja,mpango wa biashara pekee ndio wanachohitaji.
Kisha ongea na matajiri katika mji wako(angalia usitoe taarifa zote
za mpango wako mpaka upate uhakika kuwa utapata fedha-kuzuia kuibiwa
mawazo).
v . Uwekezaji Binafsi(Kuweka Akiba)
Inasemekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya bishara ndogo zonazoanzishwa huanza kutokana na akiba binafsi ya wamiliki.
Mmiliki kupitia nyenzo zilizopo za kupata kipato kama ni kazi au
biashara nyingine iliyosimama tayari anaweka akiba maalumu kwajili ya
kuanzisha biashara mpya. Kiasi cha kuanza kikifikiwa basi fedha hizo
zinaingizwa katika biashara mpya.
Fedha hizi zinaweza zikaingizwa kama mkopo binafsi ambapo baadae
zitarudishwa katika akaunti binafsi ya mmiliki au zikaingia kama
uwekezaji katika biashara ambapo mmiliki atapata faida tu
itakayozalishwa.
Vyovyote vile njia hii ni nzuri kwani hakuna madeni toka nje na unaweza ukawa na amani sana katika uendeshaji wake.
Kama wewe ni mwajiriwa na unafikiria kuwa na bishara yako basi njia hii ya kuweka akiba kwajili ya bishara yako ni njia sahihi.
Unaweza ukafungua akaunti nyingine nje na ile ya kawaida na kuhamisha
asilimia fulani kila mwezi kwenda katika akaunti hiyo ya biashara
(10-25% ni kiwango kizuri)
Ukitaka Mafanikio ni Lazima Uchukue Hatua za Haraka
Imesemwa kuwa usisubiri hadi kila kitu kikamilike ndio uanze,katika
biashara hiyo inaweza kuwa ngumu au ikakufanya usianze kabisa.
Kama tayari una mpango wa bishara unaovutia usisite kuanza kwa kukosa mtaji,chagua njia mojawapo ya kupata mtaji na uanze.
Ukitaka kupanda jengo la ghorofa ndefu,anza ngazi ya kwanza na utajikuta uko juu .
Ukisubiri kufanya yote kwa mara moja huenda usifanye kabisa.
Unapoanza kufanya kitu unapata urahisi kwa jinsi ambavyo unaenda mbele
na njia inakuwa wazi kwako katika kila hatua unayochukua.
Prosper Muro nawatakieni biashara na mafanikio mema!
No comments:
Post a Comment