MZEE MAJUTO HALI TETE… TUENDELEE KUMUOMBEA
MWEZI Mei, mwaka huu, gazeti hili la Ijumaa Wikienda liliripoti habari mbaya juu ya lejendari wa
vichekesho Bongo, Amri Athman ‘Mzee Majuto’ kuwa katika hali mbaya
kiafya, lakini kwa hali yake ilivyo kwa sasa anahitaji dua za
Watanzania.
AFANYIWA UPASUAJI
Habari mbaya zilizolifikia Amani, mapema
wiki hii zilieleza kuwa, Mzee Majuto yu kitandani kwa mara nyingine
kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa uliosababisha afanyiwe upasuaji.
Chanzo makini kililieleza Amani kuwa,
Mzee Majuto ambaye amezaliwa mwaka 1948, alilazwa kwa siku tano
hospitalini huko mkoani Tanga akisumbuliwa na ugonjwa wa hernia (ngiri)
ambapo ililazimu afanyiwe upasuaji ili kumsaidia kwenye tatizo lake hilo
la muda mrefu.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, kufuatia
tatizo hilo, Mzee Majuto amekuwa akitumia dawa za hospitalini na zile
za kienyeji, lakini hakuna unafuu wowote anaoupata.
“Kuna kipindi alilazwa hapo katikati,
alipopata nafuu aliruhusiwa lakini wiki iliyopita alibanwa sana na
unajua yule mzee alikuwa anaogopa kufanyiwa operesheni ila kutokana na
afya yake imebidi akubali tu,” kilisema chanzo chetu hicho na kuongeza:
“Kimsingi Mzee Majuto anahitaji dua za mashabiki wake na Watanzania kwa jumla.”
MKE WA MZEE MAJUTO AFUNGUKA
Baada ya kupata habari hizo, Amani lilimtafuta
msanii huyo kwa njia ya simu yake ya kiganjani ambapo ilipokelewa na
mkewe, Aisha Yusuf ambaye alithibitisha mumewe kuumwa.
Mama Majuto alisema kuwa, hadi wakati anazungumza na gazeti hili
alikuwa yupo na mumewe katika Hospitali ya Tanga Central Health Centre
(TCHC) ambako alilazwa kwa siku tano na kufanyiwa upasuaji.
“Ni kweli Mzee Majuto anaumwa ndiyo maana nimepokea simu yake, nipo
naye hapa hospitalini, anasumbuliwa na ugonjwa wa hernia ambao umeibuka
na kumuanza tena.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa
upasuaji hivyo Watanzania na mashabiki wake waendelee kumuombea na Mungu
akipenda hivi karibuni tu atarudi mzigoni, watarajie mambo mazuri
kutoka kwake,” alisema mama Majuto.
Amani lilipoomba kuzungumza na Mzee Majuto mwenyewe, mkewe alisema alikuwa usingizini kwani alitakiwa apumzike baada ya upasuaji.
“Nitamfikishia pole lakini haruhusiwi kuzungumza, anatakiwa kupumzika,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Hata hivyo, tumeambiwa tutaruhusiwa kutoka hapa hospitalini muda wowote.”
MASHABIKI WAMEMMISS
Wakiongea na gazeti hili, baadhi ya mashabiki wa staa huyo walisema
kuwa, wamemmiss sana kwenye fani yake ya uigizaji na kumuomba Mungu
afanye miujiza na amrejeshee afya yake.
“Kwa kweli tumemmiss sana, tunaamini atapona na kurejea kwenye hali
yake ya kawaida,” alisema mmoja wa mashabiki aliyejitambulisha kwa jina
la Said Juma.
UGONJWA WA HERNIA
Hernia au ngiri ni aina ya ugonjwa ambao humpata mtu baada ya misuli
au kuta za tishu mwilini zinazoshikilia au kubeba viungo (organs) fulani
kupoteza uimara au kuwa na uwazi (opening) hivyo kusababisha viungo
hivyo kutoshikiliwa ipasavyo.
Miongoni mwa vitu vinavyoweza kumsababisha mtu kupata hernia ni
pamoja na kuwa na uzito mkubwa au kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya
kubeba au kunyanyua vitu vizito, tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa
muda mrefu, ujauzito au matatizo yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa
kujifungua.
Pia kuharisha au kuvimbiwa (constipation). Vitu hivyo humfanya mtu
apate hernia ambayo husababisha afanyiwe upasuaji ili kumaliza tatizo
hilo.
No comments:
Post a Comment